
Mwimbaji wa nyimbo za injili Reuben Kigame ameishinikiza serikali kusitisha mara moja mchakato wa Mpango wa Upatanishi BBI na badala yake kuangizia masaibu wanayopitia Wakenya wakati huu wa Janga la Korona.
Kigame kupitia barua yake kwa njia ya video kwa Rais Uhuru Kenyatta, mshirika wake Raila Odinga na Katibu Mkuu wa Muugano wa Vyama wa Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli amesema huu si wakati wa kushinikiza kukusanywa kwa saini milioni moja ili kufanikisha mchakato wa kuifanyia katiba marekebisho kupitia BBI.
Kigame amesema viongozi hao wanastahili kushughulikia maslahi ya Wakenya ambao wanaendelea kufariki na kuathirika pakubwa kutokana na janga hilo.
Amewasuta viongozi hao kwa kuendeleza siasa za BBI wakati huu mgumu badala ya kuangazia masuala muhimu wakati wahudumu wa afya ambao wanategemewa pakubwa wakati huu wakifariki dunia sawa na Wakenya wengine.
Ameulaumu uongozi wa Kenyatta kwa kuwatelekeza wahudumu wa afya.
Amesema Tume ya Uchaguzi, IEBC inayostahili kuendesha kura hiyo ya maamuzi haiko tayari kwa ajili ya shughuli yenyewe.