
Shirika la Afya Duniani, WHO limetoa wito kwa mataifa ya Afrika kuwa makini zaidi kufuatia uwezekano wa ongezeko la maambukizi ya virusi vya korona wakati huu ambapo sherehe za krismasi na mwaka mpya zimekaribia.
Mkurugenzi wa WHO katika Bara la Afrika, Matshidiso Moeti amesema ongezeko la maambukizi kote duniani ni jambo la kutia wasiwasi na hali huenda ikawa mbaya zaidi watu watakapoanza kusafiri kujumuika pamoja kwa sherehe.
Kulingana na WHO, mataifa 19 yameripoti ongezeko la asilimia 20 la maambukizi katika kipindi cha siku 28 zilizopita. Aidha katika kipindi hicho kumeripotiwa ongezeko la vifo na maambukizi ya wahudumu wa afya.
Kutokana na hali hiyo, WHO imezindua kampeni kwa jina “Mask Up, Not Down” inayowalenga vijana takriban milioni 40 Afrika kuwahimiza kuvalia maski kwa njia inayostahili ili kuepusha maambukizi.