
Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli ameitaka Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC kusitisha mara moja uchunguzi inaoendesha kuhusu kisa cha afisa mmoja wa elimu kudhalilishwa na Waziri George Magoha katika Kaunti ya Kisumu.
Akizungumza na Runinga ya KTN News, Atwoli asema kwamba EACC imefeli katika majukumu yake mengine na haistahili kutumia kisa ambapo Waziri alikuwa akitekeleza majukumu yake, kunoa makali ya utendakazi wake.
Hapo jana Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Uasin Gishu, Mbaga Gitonga ambaye anadaiwa kukosewa heshima na Waziri Magoha, alihojiwa katika ofisi za EACC ambapo alitakiwa kurekodi taarifa kuelezea kilichojiri na kumsababisha Waziri Magoha kumdhalilisha hadharani.
Tayari Tume ya Huduma za Umma PSC, ilimpokonya Magoha mamlaka ya usimamizi wa wafanyakazi, hatua ambayo Magoha aliipuuza akisema kwamba ataendelea na mfumo wake wa uongozi ambao anadai umefanikisha pakubwa uboreshaji wa sekta ya elimu.
Wakati uo huo, Atwoli amewataja mawaziri Magoha, Fred Matiang'i wa Masuala ya Ndani ya Nchi na Keriako Tobiko kuwa walioonesha ukakamavu katika utendakazi wao na kusema kwamba wengine wanastahili kufutwa kazi.
<AUDIO>9989
Share this: