×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Mbunge abubujikwa na machozi akiwatetea wahudumu wa afya

Mbunge abubujikwa na machozi akiwatetea wahudumu wa afya

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kwamba serikali itashughulikia tu matakwa ya wahudumu wa afya yanayohusiana na janga la korona.

Kagwe amesema kuwa Wakenya wote kwa sasa wanapitia hali ngumu ya maisha kutokana na athari za janga hilo,  hivyo basi itakuwa vigumu kwa serikali kushughulikia matakwa mengine yasiyohusu maambukizi ya korona.

Akihojiwa na runinga moja humu nchini, Kagwe amesema malalamiko kuhusu kupandishwa vyeo, kuongezwa marupurupu na mishahara hayawezi kushughulikiwa kwa sasa.

Hata hivyo, waziri amesema kuwa serikali itahakikisha kuwa wanapewa bima ya afya endapo wataathiriwa na korona, vifaa vya kujilinda na kuboreshwa kwa mazingira yao ya kikazi.

Kagwe aidha amesema kaunti zote ambazo zinakumbwa na uhaba wa vifaa ya wahudumu wa afya kujilinda,  ziko huru kuziagiza kutoka Mamlaka ya Kusambaza Dawa KEMSA.

Ameyasema hayo saa chache baada Mbunge wa Seme James Nyakal kulia kwa uchungu wakati wa vikao vya kamati ya afya ilipokuwa ikielezwa masaibu wanayopitia wahudumu wa afya kipindi hiki cha korona.

Nyikal alibubujikwa na machozi wakati Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari KMPDU, Daktari Chibanzi Mwachonda aliposimulia jinsi wahudumu wa afya wanavyoendelea kutaabika baada ya matakwa yao kupuuzwa na serikali.

Naye Kinara wa ANC, Musalia Mudavadi amesisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kuweka mikakati ya kuwalinda wahudumu wa afya ambao wako mstari wa mbele kuwahudumia Wakenya wakati huu mgumu.

Akizungumza wakati wa misa ya wafu kwa ajili ya Daktari Robert Ayisi aliyefariki dunia kutokana na Covid-19, Mudavadi amesema awamu ya pili ya maambukizi imewaathiri pakubwa wahudumu wa afya ambao wanategemewa na taifa.

Wahudumu wa afya wametoa notisi ya kuanza kwa mgomo wao Desemba tarehe saba, iwapo matakwa yao hayatakuwa yameshughulikiwa.

Tangu kuripotiwa kwa janga la korona nchini,  jumla ya wahudumu wa afya thelathini wamefariki dunia kutokana na Covid-19 huku elfu mbili,  mia tatu sitini na tisa wakiambukizwa.