
Serikali itaanza kuwalipa maseremala ambao wamekuwa wakitengeza madawati chini ya mradi wa serikali wa shilingi bilioni 1.9 kufikia Ijumaa wiki hii.
Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema watakaolipwa ni wale ambao watakuwa wametengeneza madawati ya viwango vya ubora unaohitajika.
Akizungumza katika Kaunti ya Pokot Magharibi alipokagua jinsi mradi huo unaendelea, Magoha amesema maseremala watalipwa tu baada ya kazi zao kuchunguzwa.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika wiki ijayo.
Waziri Magoha amewahakikishia wazazi kwamba wanafunzi wako salama shuleni huku akipongeza juhudi za walimu kuendelea kuwafunza wakati huu wa janga la korona.
Magoha vile vile, amesema wakati umefika kwa Wakenya kujifunza kuishi na janga hilo na kuendelea kuzingatia maagizo ya kujilinda ikiwamo kuvalia maski.