×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Rais Kenyatta aahidi kuongeza shilingi bilioni 50 katika mgao wa kaunti

Rais Kenyatta aahidi kuongeza shilingi bilioni 50 katika mgao wa kaunti

Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kuongeza shilingi bilioni hamsini kwa mgao wa fedha za kaunti katika bajeti ya mwaka ujao.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amesema ongezeko hilo litategemea na makadirio ya mapato ya serikali kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha 2021/2022.

Rais ametoa hakikisho hilo wakati wa kikao na usimamizi wa Bunge la Seneti katika Ukulu, mkutano ambao vilevile Kinara wa ODM Raila Odinga na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya.

Ikumbuwe, kwa sasa mgao wa fedha za kaunti kutoka serikali ya kitaifa ni shilingi bilioni 316. 5 pekee, hali ambayo imechangia ugumu wa maseneta kuidhinisha mfumo mpya wa ugavi wa fedha za kaunti kutokana na uchache wake.

Wakati uo huo, Rais Kenyatta amewahimiza maseneta kuafikiana haraka kuhusu mfumo unaofaa kutumika katika kusambaza fedha katika kaunti zote, ili kukwamua shughuli ambazo zimekwama mashinani.

Wakati wa kikao hicho cha Rais, Bunge la Seneti limewakilishwa na Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio, Kiranja wa Seneti Irungu Kang'ata, Kiongozi wa Wachache James Orengo na Naibu wa Kiongozi wa Wengi Fatuma Dullo.

Wengine waliokuwapo ni Seneta Maalumu Beatrice Kwamboka na Johnes Mwashushe Mwaruma wa Taita Taveta.

Inasubiriwa kuona alasiri hii iwapo kikao hicho cha Rais kitatoa suluhu ya jinsi ya kupitisha mfumo huo ambao umekosa kuidhinishwa katika vikao tisa.

Kikao cha Rais na Usimamizi wa Seneti kimejiri wakati ambapo inaarifiwa kwamba bado maseneta hawajapata mwafaka, licha ya kupewa muda wa wiki moja kushauriana baada ya vikao kuhairishwa juma lililopita.

Inaarifiwa kwamba bado kuna mkwamo wa kupitisha mfumo huo, kwani maseneta ishirini na watano kwa jina Team Kenya wameshikilia msimamo wa kupinga, huku ishirini na wawili pekee wakiunga mkono jinsi ilivyokuwa wakati wa kikao cha tisa.

Kisheria, mfumo huo unahitaji kuungwa mkono na kupigiwa kura na angalau maseneta ishirini na wanne, hali ambayo imekuwa ngumu kwa usimamizi wa Seneti kufaulisha.