×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Watu 570 wamepona COVID-19 katika saa 24 zilizopita

Watu 570 wamepona COVID-19 katika saa 24 zilizopita

Watu mia tano na sabini waliokuwa wameambukizwa virusi vya korona wamethibitishwa kupona katika saa ishirini na nne zilizopita. Idadi hii ni ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa tangu kisa cha kwanza cha korona kuripotiwa nchini mwezi Machi mwaka huu. Hata hivyo, maambukizi  yanazidi kuongezeka huku Wizara ya Afya ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kila Mkenya kuwajibika.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema mia tano kumi na wawili ni waliokuwa wakihudumiwa nyumbani na hamsini na wanane waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali. Idadi jumla sasa ya waliopona nchini imefikia elfu tatu mia nane thelathini na sita.

Kaimu Mkurugenzi wa Matibabu Daktari Partrick Amoth, amesema wagonjwa wa COVID-19 wasioonesha dalili wataendelea kuhudumiwa nyumbani ili kupunguza gharama ya kuwahudumia hospitalini vile vile kutoa nafasi kwa hospitali nchini kutoa huduma kwa wanaozidiwa na ugonjwa huo.

Wakati uo huo,, Idadi ya walioambukizwa nchini imefikia elfu kumi na moja mia sita sabini na tatu baada ya  watu wengine mia nne ishirini na mmoja kuthibitishwa kuambukizwa katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita.

Kwingineko watu wengine wanane wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 na kufikisha idadi jumla nchini kuwa mia mbili kumi na saba.

Akizungumza kwenye Kaunti ya Nakuru, Waziri Kagwe ameendelea kuwashauri Wakenya kutii masharti ambayo yametolewa na serikali kudhibiti maambukizi huku akiwaonya vijana kuwa wao pia wako hatarini kwani virusi vya korona haviwaathiri wazee pekee ilivyodhaniwa awali.

Amesema Kaunti zina uwezo wa kuvishughulikia visa vya korona, kauli inayojiri siku moja tu baada ya Baraza la Magavana kutishia kutangaza masharti zaidi kwenye kaunti zao iwapo maambukizi yataendelea kuongezeka.

Kuhusu iwapo serikali itatangaza marufuku ya kuingia na kutoka kwenye kaunti ambazo zimerekodi idadi ya juu ya maambukizi, Waziri Kagwe amesema wananchi wana jukumu kubwa kuhakikisha hilo halitafanyika, msimamo ambao umesisistizwa na Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui.

Kwa jumla kaunti arubaini na mbili zimerekodi visa vya korona huku Nairobi ikiongoza na visa elfu sita mia nne tisini na kimoja, ikifuatwa na Mombasa ambayo imerekodi visa elfu moja mia saba na themanini na tisa na Kiambu ni ya tatu na visa mia sita arubaini, huku nakuru ikiwa na visa mia moja hamsini na tano.