array(0) { } Radio Maisha | Kenya yaripoti kifo cha kwanza cha daktari kutokana na korona
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Kenya yaripoti kifo cha kwanza cha daktari kutokana na korona

Kenya yaripoti kifo cha kwanza cha daktari kutokana na korona

Kenya leo hii imerekodi kifo cha kwanza cha daktari kutokana na ugonjwa wa Covid -19 huku akiwa miongoni mwa watu wanane ambao wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita. Aidha leo hii idadi ya maambukizi ya virusi hivyo,  ndiyo ya juu zaidi ambapo watu mia nne sabini na watatu wamethibitishwa kuambukizwa katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita. 

Serikali imeendelea kuwashinikiza wananchi kuzingatia masharti yaliyowekwa kwani kuna uwezekano mkubwa kuwa visa zaidi vitaripotiwa hasa baada ya serikali kulegeza baadhi ya masharti.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amewaongoza maafisa wengine kuchukua kimya cha dakika moja kwa heshima ya Daktari Doreen Lugaliki, aliyefariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya korona akiwa kazini.

Daktari huyo wa kike aliyekuwa mtaalam wa masuala ya uzazi , mwenye umri wa miaka 38 aliaga dunia saa arubaini na nane tu baada ya kulazwa katika hospitali moja  ya binafsi hapa jijini Nairobi.

Kifo chake kimevutia hisia nchini ikizingatiwa ndiye daktari wa kwanza kuaga dunia kutokana na COVID-19  huku Chama cha Madaktari KMPDU kikitoa wito kwa serikali kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa madaktari hasa katika hospitali za umma.

Kuna jumla wahudumu wa afya mia mbili tisini na wawili ambao wameambukizwa virusi vya korona, mia moja sitini wakiwa wanawake na wanaume wakiwa mia moja thelathini na wawili. Kaimu Mkurugenzi wa Matibabu katika Wizara ya Afya Daktari Patrick Amoth amesema wote kwako katika hali nzuri kwa sasa.

Haya yanajiri huku idadi ya walio na korona nchini ikifikia elfu tisa mia nne arubaini na nane baada ya watu mia nne sabini na watatu kuthibitishwa kuambukizwa katika saa ishirini na nne zilizopita.

Wakati uo huo,  Waziri Kagwe amesema watu sabini na sita wamethibitishwa kupona na kufikisha idadi jumla kuwa watu elfu mbili mia saba thelathini na watatu.

Kagwe kwa mara nyingine amewashauri  Wakenya kuzingatia masharti ya serikali ili kudhibiti maambukizi zaidi. Waziri huyo hasa amewapa changamoto viongozi wa makanisa kutowaruhusu watu walio na umri wa miaka  sitini na zaidi na wenye magonjwa kama vile kisukari na shinikizo la damu kuhudhuria ibada akisema wako hatarini hata zaidi. Kauli hiyo imesisitizwa na Gavana wa Kilifu Amason Kingi akisema jukumu kuu sasa ni kwa wananchi..

Wizara ya Afya imesema kwa sasa kuna jumla ya wagonjwa arubaini na wanne wa COVID -19 walio katika vyumba vya wagonjwa mahututi.