array(0) { } Radio Maisha | Watu wengine 59 wathibitishwa kuambukizwa virusi vya korona nchini Kenya
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Watu wengine 59 wathibitishwa kuambukizwa virusi vya korona nchini Kenya

Watu wengine 59 wathibitishwa kuambukizwa virusi vya korona nchini Kenya

Wizara ya Afya imetangaza kushirikiana na viongozi wa jamii vilevile mashirika yasiyo ya Kiserikali kuhamasisha jamii kuhusu mambukizi ya virusi vya korona hasa wakati huu ambapo maambukizi mengi ni katika jamii. Hayo yakijiri leo hii  idadi ya chini ya maambukizi imeripotiwa kulinganisha na siku za hivi punde japo Kaunti za Nairobi na Mombasa zinaendelea kuongoza kwa visa vya maambukizi. Aidha idadi ya wanaume wanaoambukizwa inaendelea kuwa ya juu. 

Katika hotuba hiyo ya kila siku Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Afya, Dakta Mercy Mwangangi, amesema kuwa mashirika hayo yatasaidia pakubwa hasa katika kuwaelimisha wananchi ambao wameanza kulegeza kamba kuhusu kujikinga dhidi ya maambukizi.

Akizungumzia idadi ya walioambukizwa virusi vya korona kwa kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita, Mwangangi amesema kuwa watu 59 wameambukizwa  baada  ya sampuli 2,354 kupimwa, idadi jumla  ya walioambukizwa ikiwa 4,797. Sampuli zilizopimwa kufikia sasa zikiwa elfu mia moja arubaini na mbili, mia tatau sitini na sita. Miongoni mwa walioambukizwa, 47  ni wanaume huku 12 wakiwa wanawake. Wote wakiwa Wakenya kati ya umri wa miaka 7-67.

Vilevile watu 73 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani idadi kamili ya waliopona ikiwa elfu moja mia sita themanini, huku 2 wakifariki dunia na kufikisha 125 idadi jumla ya waliofariki nchini.

Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa idadi ya maambukizi  ikiwa na visa 28, Mombasa 21, Kilifi 3, Kiambu na Machakos visa viwili kila Kaunti kisha Kisumu, Bungoma, Uasin Gishu kisa kimoja kila Kaunti.

Hayo yakijiri Serikali imeahidi kutoa taarifa kamili kuhusu utayarifu wa serikali za kaunti wa kukabili maambukizi ya virusi vya korona wiki hii.

Mwangangi amesema wamekuwa wakishirikiana na serikali zote arubaini na saba kuweka mikakati hiyo kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kuwataka magavana kuboresha maeneo ya karantini, vilevile kuwa na angalau vitanda mia tatu katika kila kaunti ili kuziwezesha kuwahudumia wananchi watakaombukizwa korona.

Kauli ya Mwangangi inajiri baada ya serikali kukosa kutoa taarifa hiyo Alhamisi wiki jana jinsi ilivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kufanya mkutano na magavana katika Ikulu hapa Nairobi. Katika mkutano huo magavana walijadili maswala mbalimbali ukiwamo utayarifu wa kukabili maambukizi vilevile mikakati ya kurejelewa kwa shughuli za kawaida.

Wakati uo huo,  Wizara ya Afya imewataka maafisa wanaohudumu kwenye maeneo ya mipaka ya Kenya na Tanzania na Uganda kuharakisha shughuli ya kuzikagua stakabadhi za madereva wa matrela ili kuepuka misongamo katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Mwangangi, hapana haja ya madereva walio na vyeti vya kuonesha hawajaambukizwa korona kuzuiwa mipakani, akisema milolongo mirefu inahatarisha maisha ya Wakenya wanaotangamana nao.