array(0) { } Radio Maisha | Watu wengine 134 waambukizwa korona nchini Kenya
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Watu wengine 134 waambukizwa korona nchini Kenya

Watu wengine 134 waambukizwa korona nchini Kenya

Idadi ya maambukizi ya virusi vya korona nchini Kenya imefikia elfu mbili mia nne sabini na nne baada ya watu wengine 134 kuthibitishwa kuambukizwa kwa kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita. Visa hivyo vimethibitishwa baada ya kupimwa kwa sampuli elfu tatu, mia moja sabini na saba. Watu 131 miongoni mwa walioambukizwa ni Wakenya huku watatu wakiwa raia wa kigeni. Aidha tisini na wanane miongoni mwao ni wa jinsia ya kiume huku thelathini na sita wakiwa wa jinsia ya kike huku visa hivi vikiwahusisha watu wenye umri wa kati ya miaka sita na sabini.  

Jinsi anavyoelezea Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Afya, Mercy Mwangangi, miongoni mwa visa hivyo, 67 vimeripotiwa Mombasa, Nairobi 31, Busia visa kumi na vitano, Machakos vitano, Taita Taveta visa vinne, Kilifi na Nakuru visa viwili katika kila eneo, huku maeneo ya Garissa, Muranga, Kisumu, Uasin Gishu na Kajiado yakiwa na kisa kimoja kimoja.

Aidha idadi ya wanaopona baada ya kuambukizwa inaendelea kuongezeka ambapo watu wengine 51 wameondoka hospitalini na kufikisha idadi jumla ya waliopona kuwa 643. Hata hivyo, mtu mwingine mmoja amefariki dunia hali inayofikisha idadi ya vifo nchini kutokana na korona kuwa 79.

Kutokana na ongezeko la maambukizi, Mwangangi amezishauri kaunti kuimarisha huduma zake za matibabu hasa baada ya kukabidhiwa shilingi takirban bilioni tano na Serikali ya Kitaifa kuwahudumia waathiriwa. Aidha amezungumzia mpango unaoendelezwa na Wizara ya Afya wa kuanza kuwahudumia nyumbani wagonjwa wasio na dalili kali za maambukizi akisema mipango yote inawekwa kuhakikisha wanahudumiwa vyema ili kuepusha maambukizi zaidi. Wataoruhusiwa kuondoka hospitalini watafuatiliwa kupitia kwa mfumo wa Jitenge APP.

Mwangangi amewashauri wananchi kuendelea kuzingatia masharti ya kujikinga mfano kunawa mikono, kutokaribiana na hata  uvaliaji wa maski ambao anasema unaweza kupunguza maambukizi kwa asilimia 50.