array(0) { } Radio Maisha | Watu wengine 72 wathibitishwa kuambukiziwa korona nchini Kenya
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Watu wengine 72 wathibitishwa kuambukiziwa korona nchini Kenya

Watu wengine 72 wathibitishwa kuambukiziwa korona nchini Kenya

Watu wengine 72 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya korona humu nchini na kufikisha idadi jumla kuwa elfu mbili tisini na watatu.

Waathiririwa ni wenye umri wa kati ya miaka kumi na mmoja na sabini na mitatu, hamsini wakiwa wanaume na wanawake ishirini na wawili.

Akitoa takwimu kuhusu  hali ya maambukizi humu nchini, Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Afya, Rashid Aman amesema maambukizi hayo mapya yamethibitishwa kufuatia kupimwa kwa sampuli elfu mbili mia nane tisini na mbili kwa kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita.

Miongoni mwa visa hivyo, 39 vimeripotiwa hapa Nairobi, Busia kumi na vitatu, Mombasa vinane, Kajiado vinne, Migori visa vitatu, Kiambu viwili sawa na Garissa huku Kisumu ikiwa na kisa kimoja.

Miongoni mwa visa vilivyothibitishwa katika Kaunti ya Mombasa, viwili viko Mvita, Changamwe viwili, Kisauni viwili, Likoni kimoja sawa na Nyali.

Kampuni ya Usambazaji wa Nguvu za Umeme Kenya Power imethibitisha kwamba wafanyakazi wake watatu ni miongoni mwa watu wa hivi punde walioambukizwa virusi vya korona katika Kaunti ya Mombasa.

Katika taarifa ya Kenya Power, kwa sasa maafisa hao wamewekwa karantini huku wakiendelea kuhudumiwa. 

Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi wengine katika ofisi ya Kenya Power mjini Mombasa, hasa walioko katika ghorofa ya kwanza, wameagizwa kusalia nyumbani kwa kipindi cha wiki moja ili wafanyiwe uchunguzi kubaini iwapo wameambukizwa korona ama la, kabla ya kurejea kazini.

 Agizo hilo limetolewa na Meneja Msimamizi, Bernard Ngungi. Aidha hali ya maambukizi katika kaunti nyingine ni kama ifuatavyo.

Vilevile kufuatia kuendelea kuongezeka kwa maambukizi katika eneo la Kibra, jijini Nairobi, Aman amesema serikali inaendelea kuyatambua maeneo ya Kibra yaliyoathiriwa zaidi kabla ya kuchukua hatua zaidi za kuzuia maambukizi.

Aman ametangaza kwamba serikali imeanza kutumia njia nyingine za kuwatambua watu takriban 140 ambao walithibitishwa kuambukizwa korona lakini hawajulikani waliko baada ya kutoa taarifa za uongo kuwahusu wakati walipopimwa. Miongoni mwa mbinu zitakazotumiwa ni nambari za vitambulisho vya kitaifa.

Idadi ya wagonjwa ambao wamepona baada ya kuambukizwa inaendelea kuongezeka huku wengine 17 wakiruhusiwa kuondoka hospitalini na kufikisha idadi jumla ya waliopona kuwa 499. Hata hivyo wagonjwa wengine wawili wamefariki dunia na kufikisha idadi hiyo kuwa 71.

Wakati uo huo, madereva wa  matrela wameonywa dhidi ya kukiuka masharti ya kuhakikisha wanapiwa takriban saa arobaini na nane kabla ya kuanza safari zao ili kuhakikisha kwamba uchukuzi wa mizigo unaendeshwa kwa njia shwari na kuepusha msongamano wa matrela hasa katika maeneo ya mipakani.