array(0) { } Radio Maisha | Duale aponea mabadiliko katika Chama cha Jubilee
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Duale aponea mabadiliko katika Chama cha Jubilee

Duale aponea mabadiliko katika Chama cha Jubilee

Rais Uhuru Kenyatta leo hii ameongoza kikao cha wabunge wa Jubilee na kufanya mabadiliko mbalimbali ya uongozi japo Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale, amesazwa katika mabadiliko hayo.

Hata hivyo walioangukiwa na shoka la mageuzi ni Kiranja wa Bunge Benjamini Washiali na Naibu wake Cecily Mbarie ambao wamevuliwa rasmi madaraka.

Rais Kenyatta amemteua Mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe kujaza nafasi ya Washiali huku Mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore akichukua nafasi ya Mbarire.

Aidha wakati wa kikao hicho Amos Kimunya ameteuliwa kuwa Katibu wa Muungano wa Wabunge wa Jubilee. 

Duale amekipongeza Chama cha Jubilee na kinara wa chama hicho, Rais Kenyatta, kwa kumpa fursa nyingine ya kuendelea kuhudumu katika wadhifa wa Kiongozi wa Wengi.

Amesema  hatua ya kusalia katika wadhifa huo ni ishara kwamba Jubilee ina imani na uongozi wake katika bunge. Awali ilitarajiwa kuwa Jubilee ingetangaza mabadiko zaidi katika uongozi wa kamati mbalimbali na kuwalenga Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichunguzwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti , David Pkosing wa uchukuzi, Julius Melly wa Elimu, Moses Kuria, Alice Wahome, Joseph Limo, na Gladys Sholei.

Duale hata hivyo amesema mabadiliko zaidi yatafanywa katika kamati za bunge ambayo yatawaathiri wanachama mbalimbali wa Jubilee. Mabadiliko hayo hasa yatawalenga wenyekiti wa kamati sawa na manaibu wao, na kwamba taarifa zaidi kuhusu mageuzi hayo zitawasilishwa kwa Spika.

Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto, Katibu Mkuu Raphael Tuju na wabunge 212 na kuondoa hofu ya awali kwamba huenda Ruto asingehudhuria.

Ikumbukwe mabadiliko pia yalifanyika katika Bunge la Seneti ambapo wandani wa Naibu wa Rais waliodaiwa kutounga mkono sera za chama wakiwamo Kipchumba Murkomen, Susan Kihika na  Kithure Kindiki  walifurushwa katika nyadhifa zao huku wengine wakiondolewa kwenye kamati mbalimbali.

Hata hivyo, katika kikao cha alasiri cha Seneti leo hii,  Kiranja wa Bunge, Irungu Kang'ata amesema mchakato wa mabadiliko bado haujakamilika rasmi, hivyo kusema uwanachama wa kamati mbalimbali ungali ulivyokuwa awali licha ya mabadiliko yaliyotangazwa.