array(0) { } Radio Maisha | Serikali yabuni Mpango wa 'Operation Kinga Korona,kukabili maambukizi zaidi

Serikali yabuni Mpango wa 'Operation Kinga Korona,kukabili maambukizi zaidi

Serikali yabuni Mpango wa 'Operation Kinga Korona,kukabili maambukizi zaidi

Serikali imebuni Kitengo Maalum cha Kushughulikia Virusi vya Korona National Multi Agency Command Centre "Operation Kinga Corona ", lengo likiwa kudhibiti maambukizi vilevile kukabili athari zinazotokana na virusi hivyo na kurejesha hali ya kawaida nchini baada ya janga hilo.

Kitengo hicho kinachozijumuisha Wizara mbalimbali, Idara za Serikali vilevile mashirika mengine yanayotoa huduma muhimu za kibinadamu, kimebuniwa kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Kitaifa ya Usalama, National Security Advisory Committee.

Kitengo hicho ambacho kinapatikana eneo la Embakasi, jijini Nairobi aidha kimejukumiwa kuyatathmini mapendekezo yanayotolewa kwa serikali kuhusu mikakati zaidi ya kukabili korona.

Aidha Meja Jenerali Ayub Matiiri ndiye ambaye atakiongoza kitengo hicho, kwa kufuatilia michango ya wizara na idara za serikali na kuwashirikisha washkadau wote ili kukabili virusi vya korona nchini.

Kufikia sasa watu mia moja ishirini na sita wameambukizwa virusi vya korona nchini baada ya watu wanne zaidi kuthibitishwa leo hii. Maambukizi ya leo aidha yanawajumuisha Wakenya watatu na raia mmoja wa Pakstani.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aidha amesema kuwa mmoja miongoni mwa wanne hao alisafiri kutoka Malawi na mwingine kutoka Pakstani kuja nchini.

Wakati uo huo Wizara ya Afya imeagiza kuongezwa muda wa siku kumi na nne kwa watu walio karantini baada ya kubainika kwamba baadhi ya watu walio karantini wamekuwa wakipuuza maagizo ya serikali hasa kujiepusha na na maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu.