array(0) { } Radio Maisha | Rais Kenyatta afanya mazungumzo na Wakenya waliopona korona

Rais Kenyatta afanya mazungumzo na Wakenya waliopona korona

Rais Kenyatta afanya mazungumzo na Wakenya waliopona korona

Rais Uhuru Kenyatta leo hii  amefanya mazungumzo ya moja kwa moja kupitia mtandao wa Zoom video akiwa Ikulu na Wakenya wawili waliokuwa katika ofisi za Wizara ya Afya ambao wamepona kabisa baada ya kuambukizwa virusi vya korona hapo awali.

Rais Kenyatta amefanya mazungumzo hayo na Brenda Cherotich mwenye umri wa miaka 27 aliyekuwa wa kwanza kuripotiwa kuambukizwa virusi hivyo nchini , vilevile mvulana kwa jina Brian Orinda ambaye aliambukizwa na Brenda baada ya kutangamana naye aliporejea nchini  kutoka Marekani.

Rais Kenyatta amempongeza Brenda kwa ujasiri aliyokuwa nao wa kujisalimisha kwa maafisa wa afya baada ya kubaini kuwa huenda alikuwa ameambukizwa.

Brenda aidha amesimulia hali ilivyokuwa kipindi alichokuwa karantini huku akiwashukuru wahudumu wa afya na wengine waliomshughulikia kipindi alichokuwa amelazwa hospitalini.

Kwa upande wake Brian amewashauri Wakenya kuzingatia maagizo wanayopewa na serikali kuhusu kujitenga ili kuhakikisha hawaambukizi.

Rais Kenyatta ameelezea matumaini kwamba vita dhidi ya maradhi ya Covid-19  vitafaulu huku akisema serikali i tayari kuweka mikakati zaidi ili kuwalinda wananchi.

Rais hata hivyo ameomba msamaha Wakenya kufuatia hatua ya baadhi ya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi katika utekelezaji wa agizo la kutopatikana nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri.