array(0) { } Radio Maisha | Serikali yaweka mikakati ya kuwafuatilia watu waliotangamana na waathiriwa wa korona Eneo la Pwani

Serikali yaweka mikakati ya kuwafuatilia watu waliotangamana na waathiriwa wa korona Eneo la Pwani

Serikali yaweka mikakati ya kuwafuatilia watu waliotangamana na waathiriwa wa korona Eneo la Pwani

Serikali imeweka mikakati ya kuwafuatilia watu waliotangamana na waathiriwa wa virusi vya korona katika eneo la Pwani ili kuhakikisha wanazingatia utaratibu uliowekwa na serikali wa kukabili maambukizi zaidi. Amesema Mshirikishi wa Utawala wa Eneo la Pwani John Elung'ata.

Katika kikao na wanahabari, Elung'ata aidha amesisitiza kwamba kaunti za Pwani zimeweka mikakati ya kutosha ya kuwashughulikia wagonjwa watakaoonesha dalili za ugonjwa wa Covid-19 ambao unaendelea kusababisha vifo vingi kote duniani.

Kulingana naye, wametenga vyumba vya kutosha vya kuwaweka karantini wagonjwa vilevile kutumia mtandao wa mulika ,ambao wakazi wa Pwani wanatumia kutoa taarifa za dalili zozote zinazofanana na za korona.

Kuhusu kutekelezwa kwa amri ya kutopatikana nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri, Elung'ata amewahakikishia wakazi wa Pwani kuwa serikali inaendelea kuweka juhudi ili kuhakikisha kwamba shughuli katika Kivuko cha Likoni Feri, zinatekelezwa.

Amesema jukumu kuu la maafisa wa usalama wakati wa kutekelezwa kwa amri hiyo ni kuwalinda Wakenya na mali zao, serikali ikiendelea kunyunyiza dawa katika maeneo kadhaa ya miji ya pwani.

Ikumbukwe, Shirika la Feri, KFS lilitangaza mikakati ya ziada ya kuhakikisha kuwa shughuli ya kuwavukisha watu katika kivuko hicho inatekelezwa kwa utaratibu zaidi.

Katika taarifa yake,  KFS, ilisema kuwa abiria watavukishwa kuanzia saa kumi na moja alfajiri hadi saa tano asubuhi, huku magari yakiruhusiwa kwenye feri kuanzia saa tano hadi saa nane mchana kabla ya abiria kuruhusiwa tena kuanzia saa nane hadi kumi na mbili unusu jioni.

Miongoni mwa kaunti tatu za pwani zilioathirika na virusi vya korona, Kilifi inaongoza kwa visa sita, ikifuatwa na Mombasa kisha Kwale.