array(0) { } Radio Maisha | Aliyefariki dunia kutokana na virusi vya korona kuzikwa Ijumaa

Aliyefariki dunia kutokana na virusi vya korona kuzikwa Ijumaa

Aliyefariki dunia kutokana na virusi vya korona kuzikwa Ijumaa

Na Caren Papai,

NAIROBI, KENYA, Maafisa wa Wizara ya Afya Ijumaa wataongoza shughuli ya kuuzika mwili wa Mkenya wa kwanza ambaye alifariki dunia kufuatia maambukizi ya virusi vya korona.

Wizara hiyo imesema mwili wa mwendazake aliyefariki dunia akitibiwa katika Hospitali ya Agha Khan jijini Nairobi, sharti uzikwe katika kipindi cha saa ishirini na moja ili kuzuia maambukizi zaidi iwapo mwili huo utapelekwa katika hifadhi ya maiti ambapo unaweza kushughulikiwa na watu wengi.

Katika taarifa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alisema mwanamume huyo Mourice Namiinda mkazi wa Kibomet- Kitale aliwasili  humu nchini kutoka Uswizi Machi 13 kisha kuanza kuonesha dalili za Covid-19.

Kagwe alisema marehemu aliyekuwa na umri wa miaka sitini na sita alikuwa akiugua ugonjwa wa kisukari. Kifo chake kilijiri siku moja baada ya Kenya kutangaza kupona kwa mwathiriwa mmoja wa virusi hivyo.

Hayo yanajiri huku idadi ya maambukizi nchini ikifikia thelathini na moja baada ya Wizara hiyo ya Afya kutangaza kuongezeka kwa waathiriwa wengine watatu.

Hata hivyo, idadi hiyo inahofiwa kwamba huenda ikaongezeka kwani kuna jumla ya watu kumi na wanane walio na dalili zonazofana na za korona ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mbagathi huku hali zao zikifuatiliwa. Aidha jumla ya watu mia tisa na sita waliotangamana na waathiriwa, wanaendelea kufuatiliwa ili kubaini iwapo wana korona au la.

Si hayo tu,  Wizara hiyo imeendelea kuitaja Kaunti ya Kilifi kuwa iliyo katika hatari kubwa  ya kurekodi visa vingi zaidi ikisema mashauriano yanaendelea kuhusu hatua zitakazochukuliwa.

Ikumbukwe wiki mbili zimekamilika, tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza cha virusi hivyo humu nchini huku muda huu ukitajwa kuwa muhimu kubaini mkondo taifa likatachukua kuhusu maambukizi na mikakati ya kuwashughulikia waathiriwa. Shirika la Afya Duniani WHO, linashauri muda huu ni muhimu kwa utekelezaji wa mikakati ya serikali  mfano kufungwa kwa shule na hata kuwekwa marufuku ya kutoka nje ili kuzuia maambukizi zaidi.