array(0) { } Radio Maisha | Viongozi mbalimbali kukatwa mishahara yao

Viongozi mbalimbali kukatwa mishahara yao

Viongozi mbalimbali kukatwa mishahara yao

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Viongozi mbalimbali nchini wanaendelea kujitokeza kutangaza mishahara yao kupunguzwa katika juhudi za kupiga jeki mikakati ya serikali kukabili janga la korona.

Hatua hii imejiri siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kukatwa kwa mshahara wake na wa naibu wake kwa asilimia 80.

Sawa tu Rais, Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amekubali mshahara wake kukatwa kwa asilimia themanini, naibu wake kwa asilimia hamsini, mawaziri wote wa kaunti hiyo kwa asilimia thelathini, nao maafisa wote wakuu wakikubali kukatwa kwa asilimia ishirini. 

Amesema agizo hilo litaendelea kutelelezwa hadi pale janga hilo litakapodhitiwa nchini.

Majaji wa Mahakama ya Juu, wamekubali mishahara yao kupunguzwa kwa asilimia 30, japo maafisa wengine wa idara ya mahakama wangali kufanya uamuzi kuhusu kupunguzwa kwa mishahara yao.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya ametangaza kwamba magavana watapunguziwa mishahara yao kwa asilimia thelathini huku manaibu wao wakipunguziwa kwa asilimia ishirini.

Kwa mujibu wa Oparanya, tangazo hilo limeafikiwa baada ya mkutano uliowajumuisha magavana na manaibu wao wa kaunti zote arubaini na saba.

Mapema Alhamisi Spika wa Seneti Ken Lusaka na Mwenzake wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi,  walisema kwamba mishahara yao itapunguzwa kwa asilimia thelathini kufuatia janga hilo. Spika Lusaka alisema ni jukumu la viongozi kuisaidia serikali kulikabili janga hilo.

Maspika hao hata hivyo , wamesema bunge litafuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba fedha hizo zitawanufaisha Wakenya.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino aidha amemwandikia Spika Muturi kumfahamisha kwamba amekubali mshahara wake kupunguzwa kwa asilimia 50,  fedha zitakazotumika kwa juhudi za kuvikabili virusi vya korona.

Mwengine ambaye amemwandikia spika ni Seneta Maalumu, Millicent Omanga ambaye amekubali mshahara wake kupunguzwa kwa asilimia hamsini ili kuwasaidia waathiriwa wa korona.

Iwapo hatua ya viongozi hao itatekelezwa, basi ina maana kwamba rais ambaye hupokea mshahara wa shilingi milioni 1.44 kila mwezi, kwa mujibu wa notisi ya gazeti rasmi la serikali , sasa atapokea mshahara wa shilingi elfu 288,000.

Hata hivyo, Naibu wake ambaye hupokea shilingi milioni 1.22 kila mwezi sasa atapokea mshahara wa shilingi 245,000.

Magavana ambao hupata mshahara wa shilingi milioni 1.1  sasa watapunguziwa hadielfu 766, 499.

Aidha, manaibu wao ambao wanalipwa shilingi elfu 728,831 sasa watapunguziwa hadi shilingi elfu 583,065. Kwa mujibu wa agizo hilo la Uhuru, mawaziri ambao kwasasa hupokea mshahara wa shilingi elfu  924,000 kila mwezi, watapokea shilingi elfu 646,000 ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya kiwango Uhuru na Ruto watapokea.

Wabunge ambao hupokea shilingi elfu 710, sasa watapokea shilingi elfu 497 kwa mwezi

Bila shaka fedha hizo zitachangia pakubwa kuendesha na kufanikisha shughuli mbalimbali za serikali ikiwamo kuimarisha juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya korona pamoja na miradi mingine ya maendeleo.