array(0) { } Radio Maisha | Duale aiomba serikali kuweka mikakati ya kuwanusuru wananchi wakati huu wa korona

Duale aiomba serikali kuweka mikakati ya kuwanusuru wananchi wakati huu wa korona

Duale aiomba serikali kuweka mikakati ya kuwanusuru wananchi wakati huu wa korona

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Adan Duale ametoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya kukidhi mahitaji ya kimsingi ya wananchi wakati huu ambapo janga la korona linaendelea kusambaratisha biashara na uchumi wa taifa.

Katika taarifa, Duale amesema serikali inastahili kuhakikisha wananchi hasa wa mapato ya chini wanapata chakula, maji safi na sabuni ili kudumisha usafi na kuzuia maambukizi ya virusi vya korona.

Kiongozi huyo wa wengi amesema bunge li tayari kufanya vikao vya dharura ili kupitisha sheria muhimu ambazo zitafanikisha vita dhidi ya korona.

Duale ametoa mfano wa mataifa mfano Marekani, Ufaransa, NewwZealand na Australia ambayo tayari yametenga fedha za kuwasaidia wafanyabiashara na wafanyakazi ambao wamesimamishwa kazi ili kujikimu wakati huu.

Amependekeza kuzinduliwa kwa hazina maalum ambayo itatumiwa kusambaza fedha hasa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo, benki kuagizwa kuondoa riba kwa mikopo yote hasa iliyoombwa na watu wasiojiweza katika jamii huku Mamlaka ya Ukusanyaji Kodi, KRA ikiombwa kuondoa kodi inayotozwa katika mishahara.

Aidha KRA imeombwa kuangazia upya kodi inazotozwa bidhaa mbalimbali na kuipunguza kwani huenda bei ya bidhaa ikapanda zaidi.