array(0) { } Radio Maisha | Idadi ya walioambukizwa Virusi vya Korona nchini yafikia kumi na sita

Idadi ya walioambukizwa Virusi vya Korona nchini yafikia kumi na sita

Idadi ya walioambukizwa Virusi vya Korona nchini yafikia kumi na sita

Idadi ya walioambukizwa Virusi vya Korona nchini imefikia kumi na sita, baada ya kisa kimoja kuripotiwa leo Jumatatu.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe amesema mwathiriwa huyo alitangamana na watu wanane waliothibitishwa jana kuwa na virusi hivyo.

Akihutubia taifa kuhusu maambukizi mapya ya korona, Kagwe amesema serikali kuu ikishirikiana na serikali za kaunti imefuatilia hali ya afya ya watu zaidi ya mia sita waliotangamana na mwathiriwa aliyethibitishwa kuwa na Korona leo.

Kagwe amesema watu tisini na sita miongoni wa mia sita hao wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kuwekwa karantini kwa siku kumi na nne bila kuonesha dalili zozote zinazofafana na za Korona.

Aidha, amethibitisha kuwa maafisa wa afya wanaendelea kufuatilia hali ya wagonjwa mia tano, huku wakiwa katika hali nzuri isipokuwa mmoja ambaye amewekwa karantini katika Kaunti ya Mombasa ambaye hali yake ya afya imezoroteka, kumi na mmoja wakiwa tayari wamefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Mbagathi wakisubiri matokeo.

Wakati uo huo amesisitiza mafuruku ya safari za ndege kutoka mataifa yaliyoathiriwa na virusi hivyo. Amesema abiria watakaowasili nchini kuanzia leo hadi Jumatano usiku wa manane watalazimika kuwekwa karantini kwa gharama zao au serikali.

Kagwe amewaonya wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma dhidi ya kuongeza nauli wanapotekeleza agizo la kupunguza idadi ya abiria hadi asilimia sitini ili kufidia hasara, akisema ni sharti wawe tayari kuathirika kifedha sawa na sekta nyingine zote nchini.

Mapema leo wahudumu wa magari ya uchukuzi wameanza kutekeleza maagizo ya serikali. Wahudumu wa magari eneo la Imara kuelekea Jijini la Nairobi wakiongeza nauli kutoka shilingi hamsini au sitini hadi shilingi themanini huku wale wanaotoka eneo la Umoja wakilazimika kulipa shilingi mia mbili kinyume na awali ambapo ilikuwa shilingi sabini.

Katika eneo la Ongata Rongai nauli iliongezwa mara dufu, abiria wakilzimika kulipa shilingi mia mbili hadi jijini Nairobi kutoka shilingi sabini.

Aidha wahudumu wa magari ya kutoka Nyeri kuja jijini Nairobi wameongeza nauli hadi shilingi mia tano, wakidai kuwa hatua hiyo itawasaidia kufidia hasara.