array(0) { } Radio Maisha | Gavana Joho aiomba serikali kufunga mipaka yote

Gavana Joho aiomba serikali kufunga mipaka yote

Gavana Joho aiomba serikali kufunga mipaka yote

Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho ameiomba serikali kufunga mipaka yake kabisa kwa siku kumi na nne ili kuepuka maambukizi zaidi ya virusi vya korona.

Kwa mujibu wa gavana huyo, kufungwa kwa mipaka na kusitishwa kwa safari za ndege zinazotua na kwenda katika mataifa ya nje kutalisababishia taifa hili hasara ila ni sharti serikali ichukue hatua.

Kauli yake inajiri baada ya Shirika la Ndege la Kenya Airways kuthibitisha kwamba litasitisha safari zote za ndege kufikia saa sita usiku Jumatano wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapisha katika mtandao wa Twitter, KQ imesema kwamba safari hizo zitasitishwa kikamilifu hadi pale hali ya kawaida itakaporejelewa. Aidha, imeongezea kwamba wateja wao ambao wataathirika na kusitishwa huko, wako huru kuchagua tarehe nyingine ya kusafiri chini ya kipindi cha miezi kumi na miwili ijayo.

Hatua hiyo inafuatia agizo la serikali la kusitisha safari zote za kimataifa baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya korona kutoka 7 hadi 15.

Vilevile gavana huyo amesikitishwa na hulka za Wakenya pamoja na viongozi kupuuza maagizo yanayotolewa na serikali hata wakati ambapo taifa linakumbwa na virusi ambavyo havijawahi kushuhudiwa duniani. Amewataka viongozi wa makanisa pamoja na wale wa dini ya Kiislamu kuhakikisha maeneo ya kuabudu yanasalia kufungwa ili kuepuka virusi hivyo.

Wakati uo huo, viongozi wameshauriwa kuwahamasisha wakazi wao kuhusu virusi hivyo.