array(0) { } Radio Maisha | KQ kusitisha safari za ndege Jumatano wiki hii

KQ kusitisha safari za ndege Jumatano wiki hii

KQ kusitisha safari za ndege Jumatano wiki hii

Shirika la Ndege la Kenya Airways limethibitisha kwamba litasitisha safari zote za ndege kufikia saa sita usiku Jumatano wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapisha katika mtandao wa Twitter, KQ imesema kwamba safari hizo zitasitishwa kikamilifu hadi pale hali ya kawaida itakaporejelewa. Aidha, imeongezea kwamba wateja wao ambao wataathirika na kusitishwa huko, wako huru kuchagua tarehe nyingine ya kusafiri chini ya kipindi cha miezi kumi na miwili ijayo.

Hatua hiyo inafuatia agizo la serikali la kusitisha safari zote za kimataifa baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya korona kutoka 7 hadi 15.

Taarifa ya KQ inajiri siku kadhaa baada ya nyingine iliyodokeza kwamba wakuu wa shirika hilo pamoja na wafanyakazi watalazimika kupunguziwa mishahara ili kujikimu huku wafanyakazi wengine wakitakiwa kuenda likizo ya lazima bila malipo kuanzia tarehe mosi mwezi ujao.