array(0) { } Radio Maisha | Meja Jenerali Mohammed Abdalla Badi kusimamia Nairobi Metropolitan Services NMS

Meja Jenerali Mohammed Abdalla Badi kusimamia Nairobi Metropolitan Services NMS

Meja Jenerali Mohammed Abdalla Badi kusimamia Nairobi Metropolitan Services NMS

Rais Uhuru Kenyatta amemteua Meja Jenerali Mohammed Abdalla Badi kusimamia baadhi ya majukumu ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi yaliyohamishiwa Serikali Kuu. Badi ataongoza Majukumu ya Jiji chini ya Kitengo kipya ambacho kimebuniwa yaani Nairobi Metropolitan Services, NMS.

Akizungumza baada ya majukumu hayo kuhamishiwa rasmi Serikali Kuu leo hii, Rais Kenyatta aidha amemteua Enosh Onyango Momanyi kuwa Naibu wa Badi.  

Kenyatta amekishauri kitengo hicho kuukabili ufisadi ambao umelameza shughuli katika Kaunti ya Nairobi. Ametaja sekta mbalimbali ambazo zimeathirika na usimamizi mbaya zikiwamo, uchukuzi, uzoaji taka, afya na maji.

Amekipa kitengo hicho siku mia moja kuweka mikakati ya kuzishughulikia changamoto hizo.

Miongoni mwa majukumu ambayo yamehamishiwa Serikali Kuu ni Muundo-msingi, Uchukuzi, Ukusanyaji Kodi na Huduma za Umma. Hafla ya kuyahamisha majukumu hayo rasmi imefanyika katika Ikulu ya Nairobi baada ya umma kuhusishwa ambapo Gavana Sonko na Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa wametia saini mkataba na idara mbalimbali zinazohusika kama vile Tume ya Huduma za Umma ,PSC na Mamlaka ya ukusanyaji Kodi, KRA.

Maafisa wengine waliokuwapo wakati wa hafla hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kihara Kariuki, Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinywa na Spika wa Seneti Ken Lusaka.