array(0) { } Radio Maisha | Kaunti haziko tayari kuvikabili Virusi vya Korona -Oparanya

Kaunti haziko tayari kuvikabili Virusi vya Korona -Oparanya

Kaunti haziko tayari kuvikabili Virusi vya Korona -Oparanya

Kinyume na ilivyotangaza na serikali wiki hii kwamba kaunti 35 nchini zimejiandaa kukabili virusi vya korona, Baraza la Magavana limetoa taarifa inayoonesha kwamba kaunti zote nchini haziko tayari kukabili virusi hivyo. Baraza hilo limelalamikia ukosefu wa fedha za kutoka, ukosefu wa vifaa na kutokuwapo mafunzo kwa maafisa wa afya katika kaunti kuhusu namna ya kukabili Korona.

Baraza hilo limelalamikia ukosefu wa fedha na vifaa vya kupimia virusi vya korona. Mwenyekiti wa Baraza hilo, Wycliffe Oparanya amesema kaunti zimepokea vifaa 2,805 pekee vya kujikinga badala ya 305,000 vilivyotarajiwa. 

Badaza hilo aidha limelalamikia suala kwamba serikali za kaunti hazina uwezo wa kupima maambukizi ya Korona, ambapo Oparanya amesema kwamba kuna maabara mbili pekee za kushughulikia virusi hivyo kote nchini. Ameongeza kwamba ni sharti kaunti zote ziwe na uwezo wa kupima wagonjwa wanaoonyesha dalili za virusi hiyo badala ya kutumwa kwa sampuli hadi Nairobi na kisha majibu kurejeshwa mashinani.

Wakati uo huo, Oparanya amemtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuagiza kupewa mafunzo kwa wahudumu zaidi wa afya kuhusu jinsi ya kutambua na kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo pamoja na kugatuliwa kwa shughuli nzima ya kupimwa kwa wanaoshukiwa kuugua. Kauli hiyo imesisitizwa na magavana wenza wakiwamo Wycliffe Wangamati wa Bungoma, Joseph Ole Lenku wa kajiado, Alfred Mutua wa Machakos na Martin Wambora wa Embu.