array(0) { } Radio Maisha | Idadi ya walioambukizwa Korona imefikia 7, Kenya

Idadi ya walioambukizwa Korona imefikia 7, Kenya

Idadi ya walioambukizwa Korona imefikia 7, Kenya

Watu watatu zaidi wamethibitishwa kuambukizwa Virusi vya Korona nchini na kufikisha 7 idadi ya walioambukizwa. Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe amesema miongoni mwa walioambukizwa ni wapenzi wawili raia wa Uhispania ambao walikuja nchini kutoka Madrid Uhispania na raia wa Burundi ambaye aliwasili nchini Machi 17 na kugunduliwa katika Uwanja wa Ndege wa JKIA kwamba ameambukizwa baada ya kufanyiwa ukaguzi. Wote walioambukizwa kufikia sasa waliingia nchini kutoka mataifa mbalimbali.

Ili kusisitiza umuhimu wa watu wanaoingia nchini kujitenga kwa kipindi cha siku 14, Waziri Kagwe ameutaka umma kumripoti mtu yeyote ambaye anakiuka masharti ya kujitenga ili aadhibiwe kwa mujibu wa sheria. Anayekiuka maagizo hayo anaweza kuhukumiwa jela.

Kagwe aidha amesema wahudumu wa afya humu nchini na wengine wa mataifa takirban ishirini leo hii wamepewa mafunzo maalum na wenzao wa Uchina kupitia mawasiliano ya moja kwa moja kupitia video ya mtandao na kuelimishwa kuhusu namna ya kuvishughulikia visa vya Korona. Amesema miongoni mwa masuala makuu yaliyosisitizwa ni kuzingatia usafi kwa kunawa mikono na watu kujiepusha na makongamano.

Baadaye leo serikali itatoa maagizo zaidi kuhusu mambo muhimu yanayostahili kutekelezwa nchini ili kuzuia maambukizi zaidi.