array(0) { } Radio Maisha | Bunge la Kitaifa na seneti yaahirisha vikao kufuatia Korona

Bunge la Kitaifa na seneti yaahirisha vikao kufuatia Korona

Bunge la Kitaifa na seneti yaahirisha vikao kufuatia Korona

Katika mojawapo ya juhudu za kuzuia visa vya maambukizi zaidi ya virusi ya Korona, Mabunge ya Kitaifa na Seneti yamesitisha vikao vyake kwa kipindi cha siku kumi na tisa.

Spika wa Bunge hilo Justin Muturi alitangaza rasmi kusitishwa kwa vikao hivyo jana jioni akisema kwamba Bunge hilo litafunguliwa tena tarehe 14 mwezi Aprili mwaka huu na kwamba hatua hiyo inaendana na wito wa Rais Uhuru Kenyatta wa kusitisha shughuli mbalimbali ili kuvikabili virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid - 19.

Ikumbukwe kuwa Idara ya Mahakama ndiyo iliyokuwa ya kwanza kusitisha huduma zake huku Jaji Mkuu David Maraga akitoa muongozo kuhusu kesi ambazo ni za dharura pamoja na kutoa wito wa baadhi ya kesi ndogo ndogo kusuluhishwa katika vituo vya polisi.

Hoja ya kusitishwa kwa vikao hivyo iliwasilishwa na kiongozi wa Wengi Aden Duale ambaye pia alitumia fursa hiyo kutoa wito wa kubuniwa kwa hazina maalum ya kuwalinda wafanyabiashara wadogo wadogo nchini ambao wataathirika kutokana na kusitishwa kwa shughuli mbalimbali.

Wakati wa vikao hivyo vya jana, wabunge walishinikiza kutimuliwa bungeni kwa Mbunge wa Eldas, Adan Keynan wakidai kwamba alikuwa amewasili nchini kutoka London hivyo kustahili kuwa karantini kwa kipindi cha siku 14.

Mbunge wa Endebes, Robert Pukose alimwomba Spika Justine Muturi kumfurusha mbunge huyo kwa ajili ya afya za wenzake.