array(0) { } Radio Maisha | Wakenya walioko Uchina watumiwa fedha za matumizi

Wakenya walioko Uchina watumiwa fedha za matumizi

Wakenya walioko Uchina watumiwa fedha za matumizi

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Huku Wakenya walioko Uchina wakiendelea kuiomba serikali kuwarejesha kufuatia kusambaa kwa Virusi vya Corona, Msemaji wa Serikali kanali Mstaafu Cyrus Oguna amesema shilingi milioni 1.3 zimetolewa kuwasaidia wanafunzi zaidi ya mia moja waliokwama jijini Wuhan. Wengine watakaonufaika na msaada huo wa serikali ni wasanii tisa.

Hata hivyo amesema hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyeambukizwa Virusi vya Corona akisisitiza kwamba wanafunzi wa Kenya walioko nchini humo wanashughulikiwa.

Amesema Wakenya wawili walioripotiwa kuwa wajawazito nchini humo wanahudumiwa na kupuuza madai kwamba serikali imewatelekeza.

Akizungumza siku moja baada ya Wizara ya Afya kusema visa vyote kumi na vitatu vilivyoripotiwa nchini havihuishwa na Corona, Oguna amesema ukaguzi umeimarishwa katika maeneo takriban thelathini na manne ambayo hutumiwa na watu kuingia nchini.

Amesema ukaguzi umeimarishwa katika Uwanja wa Ndege wa JKIA vilele bandari ya Mombasa ambayo ni maeneo makuu yanayotumiwa na wageni kuingia nchini.
 
Kando na hayo, Oguna vilevile amezungumzia kero la nzige nchini akisema serikali kufikia sasa inatumia ndege 9 kuwakabili nzige ambao wameziathiri kaunti 18 kufikia sasa.

Ndege tatu zinatumiwa kunyunyiza dawa katika Kaunti ya Wajir huku nyingine zikiwa katika kaunti za Isiolo, Marsabit na eneo la Masinga huku serikali ikiwa na mipango ya kuwa na jumla ya ndege ishirini ya kuendesga shughuli hiyo.

Licha ya awali kuripotiwa kwamba nzige wamesambaa hadi katika eneo la Muhoroni kwenye Kaunti ya Kisumu, Oguna amesema imebainika wadudu walioonekana si nzige.