array(0) { } Radio Maisha | Serikali yawahakikishia Wakenya kwamba hakuna kisa cha virusi vya Corona Kenya

Serikali yawahakikishia Wakenya kwamba hakuna kisa cha virusi vya Corona Kenya

Serikali yawahakikishia Wakenya kwamba hakuna kisa cha virusi vya Corona Kenya

Wizara ya Afya imefafanua kwamba hakujakuwapo na kisa chochote cha mkenya au raia wa kigeni humu nchini kuripotiwa kuugua virusi vya Corona.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo hii Wizara hiyo imesema visa kumi na vitatu ambavyo vimeripotiwa nchini tangu virusi hivyo kuzuka nchini Uchina uchunguzi umebainisha kwamba hakuna yeyote nchini anayeugua Ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi hivyo. Wizara hiyo imesisitiza kwamba imeweka mikakati kuzuia virusi hivyo kusambaa nchini.

Miongoni mwa mikakati yenyewe ni kubuniwa kwa kamati maalum inayowahusisha maafisa wa vitengo mbalimbali walio na ujuzi wa kuukabili ugonjwa wa COVID-19.

Mpango wa kuuhamasisha umma kuhusu namna ya kuvikabili iwapo vitaripotiwa nchini, kubuniwa kwa kitengo cha dharura chenye maafisa walio na jukumu la kufuatilia na kuchunguza kisa chochote ambacho kinaripotiwa nchini, kuwekwa kwa vifaa vya kutosha katika vituo maalum vya kuchunguza virusi hivyo na kuwachunguza wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka mataifa mengine.

Mikakati mingine ni kutoa mafunzo kwa maafisa wote wa afya katika vituo vya afya vya umma na binafsi huku kufikia sasa tayari maafisa mia tano wamefunzwa.

Vituo maalum vimetengwa  katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na Mbagathi ili kushughulikia visa vyovyote ambavyo huenda vikaripotiwa nchini kando na kununua vifaa elfu tano vya kujikinga vinavyohitajika, shughuli inayoendeshwa na serikali kuu na Shirika la USAID.

Wizara ya afya pia imeushauri umma kuwa makini na kudumisha usafi. vile vile wananchi wameshauriwa kupiga ripoti kupitia nambari 0800721316 au 0732353535 iwapo wanamshuku mtu yeyote kuwa na virusi vya Corona.

Kulingana na takwimu za shirika la Afya Duniani WHO , jumla ya watu elfu mbili wamefariki dunia na wengine elfu sabini na tatu mia tatu thelathini na wawili wakiambukizwa.