array(0) { } Radio Maisha | Ruto amejitenga na sakata ya ufisadi inayohusu ofisi yake

Ruto amejitenga na sakata ya ufisadi inayohusu ofisi yake

Ruto amejitenga na sakata ya ufisadi inayohusu ofisi yake

Naibu wa Rais William Ruto anaendelea kufoka kuhusu ofisi yake kuhusishwa katika sakata ya utoaji tenda ya ununuzi wa vifaa vya kijeshi. Siku moja baada ya kujitenga na sakata hiyo kupitia mtandao , Ruto  ameendelea kujitetea  na kusema Ofisi ya Naibu wa Rais aihusiki na ununuzi wa vifaa katika Wizara wala idara yoyote ya serikali.

Ruto ameuliza swali Je, kando na mkutano wa dakika ishirini na tatu unaosemekana kufanyika ofisini mwake, wakati wa kipindi chote sakata hiyo inadaiwa kuendelea, ni ofisi zipi za serikali zilizohusika na kutembelewa na washukiwa

Ruto amesema kuna maswali kadhaa yanayostahili kujibiwa kwa mfano; Je, walifika katika Idara ya Ulinzi Nani alipanga walikutana na nani  Amesema kuna haja ya ukweli kujulikana na mbali  madai yanayotolewa katika vyombo vya habari akidai yamepangwa.

Hapo jana Ruto alidai kwamba hatua ya kumuhusisha na sakata hiyo inayosemekana kuongozwa na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa ni njama ya mahasimu wake wa kisiasa.

Jumaa iliyopita maafisa wa Idara ya Upelelezi DCI walifanya msako katika ofisi ya Ruto na kuchukua vifaa zikiwamo kanda zilizonaswa na Kamera za CCTV kwa uchunguzi zaidi. Aidha inaarifiwa baadhi ya maafisa wakuu katika ofisi hiyo ya Ruto watahojiwa. Maafisa hao ni  Msaidizi wa binafsi wa Naibu Rais Farouk Kibet Katibu wake Reuben Maiyo na Mkuu wa Wafanyakzi Ken Osinde.

Echesa alikamatwa Alhamisi iliyopita kisha kufikishwa mahakamani Ijumaa ambapo alikana za tuhuma za kumlaghai mfanyabiashara wa Marekani shilingi zaidi ya bilioni thelathini na tisa.

Inaarifiwa Echesa ambaye anazuiliwa katika korokoroni Muthaiga alitumia jina la Naibu wa Rais William Ruto na Waziri wa Ulinzi Monica Juma akisema angemsaidia mfanyabiasahara huyo kupata kandarasi ya kusambaza vifaa hivyo kwa kuwaandikia akijitambulisha kuwa mwanasiasa wa humu nchini ambaye ni rafiki wa Naibu wa Rais William Ruto.

Kandarasi hiyo inaaminika kuwa ya  shilingi bilioni 39.5. 

Ikumbukwe Mkurugenzi wa Idara ya Upelelzi  DCI, George Kinoti alisema wote waliotajwa katika stakabadhi zilizopatikana akiwamo Waziri Monica Juma watahojiwa.  Washukiwa wengine waliokamatwa ni Kennedy Oyoo, Daniel Otieno na Clifford Okoth.