array(0) { } Radio Maisha | Sekta ya elimu imedorora sasa ikilinganishwa na wakati wa Hayati Moi, asema Sossion

Sekta ya elimu imedorora sasa ikilinganishwa na wakati wa Hayati Moi, asema Sossion

Sekta ya elimu imedorora sasa ikilinganishwa na wakati wa Hayati Moi, asema Sossion

Maafisa wakuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu, KNUT wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Wilson Sossion wamefika katika majengo ya bunge kuutazama mwili wa aliyekuwa Rais wa pili Hayati Daniel Toroitich Arap Moi.

Akizungumza baada ya kuutazama mwili huo, Sossion amempongeza Mzee Moi kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za walimu wakati alipokuwa uongozini.

Sossion amesisitiza kwamba tofauti na sasa, sekta ya elimu imesahaulika hasa ikizingatiwa masaibu wanayopitia walimu nchini.

Aidha, katibu huyo amesema Moi alihakikisha kwamba maslahi ya wanafunzi yanazingatiwa kote nchini kwa kutembelea shule mbalimbali kujua changamoto wanazopitia. Vilevile amekiri kwamba tofauti na sasa, Mzee Moi aliwateua watu wenye tajriba kuongoza Wizara ya Elimu ili kufanikisha viwango vya juu kwa wanafunzi.

Sossion ameeleza kusikitishwa na jinsi Wizara ya Elimu inavyoendesha shughuli za elimu bila kuwahusisha wafanyakazi wa nyanjani. Kwa mujibu wa Sossion, Moi alifanya juhudi kuwasiliana na wakurugenzi wa elimu ili kuepuka visa vinavyoweza kuwaathiri wanafunzi.

Wakati uo huo, Sossion ameitaka serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata viwango vya juu vya elimu kwa kuwahusisha walimu kikamilifu. Pia amemwomba Waziri George Magoha kufanya ukaguzi ili kuondoa mtandao wa matapeli, cartels katika sekta ya elimu kwa manufaa ya wanafunzi na walimu.

Shughuli hiyo ya kuutazama mwili wa Moi umeingia siku ya tatu leo hii baada ya kuanza Jumamosi wiki iliyopita. Wakenya wa matabaka mbalimbali wamemiminika bungeni kuanzia Jumamosi kuutazama mwili huo. Jumamosi Wakenya takriban elfu ishirini waliutazama mwili huo huku watu elfu hamsini wakitazama jana.

Kwa jumla Wakenya elfu sabini wameutazama mwili huo ambao kesho unatarajiwa kupelekwa hadi Uwanja wa Nyayo ambapo ibada maalumu ya wafu itafanyika. Marais zaidi ya kumi wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo kabla kuhudhuria mazishi nyumbani kwake Kabarak kwenye Kaunti ya Nakuru Jumatano wiki hii.

Ikumbukwe Mzee Moi alifariki dunia Jumanne wiki jana katika Nairobi Hospital akiwa na umri wa miaka tisini na sita.