array(0) { } Radio Maisha | Jumanne 11 Februari yatangazwa kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa

Jumanne 11 Februari yatangazwa kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa

Jumanne 11 Februari yatangazwa kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa

Na Beatrice Maganga,

NAIROBI, KENYA, Waziri wa Masuala ya Ndani ya nchi, Dkt. Fred Matiang'i amechapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali siku ya Jumanne kuwa ya mapumziko ya kitaifa, ili kuwaruhusu Wakenya kumwomboleza Rais wa pili wa Kenya, Hayati Mzee Daniel Toroitich Arap Moi.

Akizungumza wakati wa kutoa ratiba rasmi ya mazishi hayo katika Jumba la Harambe jijini Nairobi, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua amesema siku hiyo imetengwa ili kuwarusu Wakenya kumwomboleza Hayati Mzee Moi, wakati wa Ibada ya Kitaifa ya wafu.

Aidha, Kinyua amesema mwili wa Hayati Mzee Moi utawekwa katika Majengo ya Bunge, kuanzia siku ya Jumamosi saa nne hadi Jumatatu ili kuwapa fursa Wakenya kuutazama kati ya saa mbili na saa kumi na moja.

Kinyua ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati andalizi, amesema Rais Uhuru Kenyatta akiwa Amiri Jeshi Mkuu, ataongoza gwaride maalumu la vikosi vyote vya majeshi, nje ya Majengo ya Bunge kwa heshima ya Mzee Moi siku ya Jumamosi asubuhi. Familia ya Moi itaandamana na majeshi hayo ambayo yatalibeba jeneza la Mzee Moi, likiwa limefunikwa na Bendera ya Kenya.

Ibada ya Kitaifa itafanyika Jumanne juma lijalo katika Uwanja wa Nyayo, ambapo marais na wageni mashuhuri kutoka ngazi za kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria.

Vilevile, amesema mazishi ya Hayati Mzee Moi siku ya Jumatano yatakuwa mazishi kamili ya kijeshi katika Boma lake la Kabarak, Kaunti ya Nakuru, ambapo mwili utakuwa chini ya ulinzi mkali huku wanajeshi wakiratibiwa kulipua mizinga kumi na tisa kwa heshima yake.