array(0) { } Radio Maisha | Moi aliimarisha kilimo; wamesema Wakenya

Moi aliimarisha kilimo; wamesema Wakenya

Moi aliimarisha kilimo; wamesema Wakenya

Kilimo kikiwa uti wa mgongo wa taifa hili, wakulima Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanamkumbuka  Hayati Daniel Toroitich Arap Moi jinsi alivyotilia maanani ukulima.

Mkulima kwa jina Henry Koech anasema juhudi zake za kuanzisha Shirika la Ustawishaji Kilimo Nchini, ADC, zililenga kuwashirikisha wakulima kupitia kusaini mkataba wa kuzalisha mbegu bora ambazo  ziliuzwa kwa Kampuni ya Kenya Seed na baadaye kwa mkulima nchini vilevile mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Koech anasema baadaye, Moi alianzisha maonesho ya kitaifa ya kilimo yaliyolenga kuwahamasisha wakulima kuhusu mbinu bora za ukulima na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa sawa na kuangazia hatua zilizopigwa na serikali yake katika kupiga jeki sekta hiyo muhimu.

Anasema Moi alianzisha sera ya kuhakikisha maafisa wa nyanjani wa kilimo wanawatembelea wakulima mashambani mwao kuwafunza kuhusu mbinu bora za kilimo kinyume ilivyo sasa.


Moi vilevile anakumbukwa kwa kuzuru ghafla maeneo yaliyokumbwa na mmomonyoko wa udongo na wakati mwingine kushiriki moja kwa moja kujenga kuta za kuzuia hali hiyo kutokea. Aidha, alitilia mkazo umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miche jinsi anavyoeleza mkulima kwa jina Julius Laibich.

Mourice Cherongony, Meneja wa ADC Ukanda ya Bonde Ufa, anasema Moi alizuia unyakuzi wa ugawanyaji wa mashamba hayo ya kilimo ili kuhakikisha mashirika kama vile lile la mbegu yanalindwa.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa kaunbti hii, Daktari Stanley Kenei anasema kuanzishwa kwa 4K Clubs shuleni vilivyomaanisha kuungana, kufanya, kusaidia Kenya kulifanikisha malengo ya kukuza kilimo nchini.


Kenei alianzisha viwanda na kuvijenga vingine vya pamba na kahawa ili kuimarisha uchumi wa taifa.

Hata hivyo anasema kuhalalisha soko huru kuliathiri sekta hiyo muhimu.