array(0) { } Radio Maisha | Akaunti za benki za Sonko kufunguliwa

Akaunti za benki za Sonko kufunguliwa

Akaunti za benki za Sonko kufunguliwa

Ni afueni kwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko baada ya Taasisi ya kutwaa Mali iliyoibwa, Assets Recovery Agency kuagiza kufunguliwa kwa akaunti tano za benki za kiongozi huyo anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi ambazo zilikuwa zimethibitiwa kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita.

Agizo hilo linafuatia wito wa mawakili wake; Harrison Kinyanjui, Cecil Miller na George Kithi ambao wameiambia mahakama kwamba muda uliokuwa umeitishwa na Taasisi hiyo wa kuzichunguza akaunti hizo umekamilika huku mteja wao akiendelea kutaabika kwa kukosa fedha za kujikimu.

Aidha, mawakili hao wamemwambia Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani Martha Mutuku kwamba taasisi hiyo vilevile haikufika mahakamani kuomba muda zaidi wa kuendeleza uchunguzi wao.

Awali, Sonko alilalamikia kuthibitiwa kwa akaunti zake akisema kwamba hakuwa na uwezo wa kuikimu familia yake kwani hata mshahara wake kama gavana ulikuwa umethibitiwa.

Gavana huyo pamoja na wafanyakazi wengine wa Kaunti ya Nairobi wanakabiliwa na mashtaka ya kufujwa kwa kima cha shilingi milioni mia tatu hamsini na saba japo wote wamekanusha tuhuma hizo.