array(0) { } Radio Maisha | Kimengich aidhinishwa rasmi kuiongoza Dayosisi ya Eldoret

Kimengich aidhinishwa rasmi kuiongoza Dayosisi ya Eldoret

Kimengich aidhinishwa rasmi kuiongoza Dayosisi ya Eldoret

Zaidi ya waumini elfu kumi  wa Kanisa Katoliki wamekusanyika pamoja na wa madhehebu mengine na viongozi wa kisiasa katika uwanja wa Shule ya Upili ya Mother of Apostle mjini Eldoret kushuhudia kuidhinishwa rasmi kwa Askofu Dominic Kimengich  kuchukua uongozi wa Dayosisi ya Eldoret.

Ilikuwa ni shangwe na vigelegele waumini wa Kanisa Katoliki wakishangilia kuidhinishwa kwa askofu Kimengich kuiongoza Dayosisi ya Eldoret baada ya uteuzi uliofanywa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Mtakatifu Francis  mwezi Novemba mwaka jana miaka miwili baada ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo Marehemu Cornelius  Korir kuaga dunia.

Kabla ya kuidhinishwa kwa askofu huyo barua ya Papa Francis akimpa Kimengich mamlaka ya kuiongoza Dayosisi ya Eldoret  kwa jina la kimombo ’ Bull’ ilisomwa kisha askofu huyo akakiri Imani yake kwa mujibu wa imani ya kanisa hilo.

Baada ya hiyo Askofu Kimengich alipewa fimbo ya uchungaji ishara kwamba ameitikia wito wa kuwa mchungaji wa kondoo, ambao ni wana wa Mungu.

Aidha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Nchini Kadinali John Njue alimwongoza  Kimengich kuketi kwenye Kiti cha Askofu ‘Cathedra’ na kumuidhinisha rasmi kuwa askofu wa Dayosisi ya Eldoret.

Akihutubu baada ya kumidhinisha Kadinali Njue alimshauri Askofu Kimengich kujikakamua kuhakikisha kuwa anaendeleza shughuli za jimbo ipasavyo.

Maaskofu wengine wa Kanisa Katoliki walimpongeza Askofu Kimengich kwa uteuzi wake wakielezea Imani kuwa ataweza kuliongoza jimbo hilo na kufuata nyayo za mwendazake Cornelius Korir

Askofu Korir anakumbukwa kwa juhudi zake za kuukabili ukabila na kuhubiri amani hasa baina ya jamii za Pokot Marakwet na Turkana ambazo zilizozna kwa muda mrefu.

Askofu Kimengich amewahakikishia waumini kuwa atafuata nyayo hizo.

Waumini wa kanisa hilo aidha wamemtunuku Askofu Kimengich gari aina ya v8 ngamia moja mbuzi 20 miongoni mwa zawadi nyingine.

Aidha ametawazawa kuwa Mzee wa Jamii ya Kalenjin

Macho yote sasa yameelekezwa kwa Askofu Kimengich ikizingatiwa kuwa Dayosisi ya Eldoret inalojumuisha Kaunti za Uasin Gishu Nandi na Elgeyo Marakwet na ni miongoni mwa Dayosisi  kubwa zaidi nchini yenye waumini wengi