array(0) { } Radio Maisha | Nobody can stop BBI Reggae, asema Raila

Nobody can stop BBI Reggae, asema Raila

Nobody can stop BBI Reggae, asema Raila

Nobody Can Stop Reggae ndio wimbo ambao umemkaribisha Kinara wa ODM, Raila Odinga jukwaani katika mkutano wa nne wa kuijadili ripoti ya Mpango wa Upatanishi, BBI kwenye Kaunti ya Kitui.

Kwa mujibu wa Raila, hakuna atakayezuia meli ya BBI ambayo tayari imeng'oa nanga. Raila amesisitiza kwamba sharti viongozi fisadi wakabiliwe kwa mujibu wa sheria hivyo wanaopinga BBI wanalenga kulemaza vita dhidi ya ufisadi.

Kwa upande wake Kinara wa Chama cha WIPER, Kalonzo Musyoka ameendelea kumpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuzidisha vita dhidi ya ufisadi.

Wakati uo huo, Raila kwa mara nyingine amepuuza kauli za baadhi ya viongozi kwamba BBI inalenga kuwatengea watu fulani nyadhifa za uongozi. Amesisitiza kwamba lengo kuu la BBI ni kuhakikisha Wakenya wote wanajumuishwa serikalini hivyo uongozi katika ngazi za juu sharti upanuliwe. Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli.

Kadhalika Raila ametumia fursa hiyo kuirai serikali kuhakikisha wakazi wa Ukambani hasa wa Kitui wanasambaziwa maji kwa asilimia zaidi ya arubaini hasa ikizingatiwa kaunti hiyo iko katikati ya mito miwili, Athi na Tana.

Licha ya nyimbo na hadithi za Raila, mkutano wa BBI awamu ya Ukambani umekumbwa na changamoto si haba. Kulikuwa na mkanganyiko wa ratiba kuanzia mwanzo huku viongozi wengine wakiwamo wa eneo hilo wakikosa kuhudhuria. Viongozi hao ni pamoja na Gavana wa Machakos Dakta Alfred Mutua ambaye yuko nje ya nchi.

Wengine ni, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jrn, Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetangula.

Mkutano huo wa BBI utasalia Ukambani, viongozi wakitarajiwa katika Uwanja wa Wote Kaunti ya Makueni Jumamosi wiki ijayo. Swali likiwa ni kwa nini mikutano miwili kwenye eneo la Ukambani Ikumbukwe kumekuwapo mvutano wa viongozi eneo hilo huku wandani wa Kalonzo wakihisi kutengwa katika mchakato mzima wa BBI. Licha ya Ngilu kuteuliwa kuongoza ngoma ya BBI Ukambani, Kalonzo vilevile yu mstari wa mbele kuirindima ngoma hiyo akitarajiwa kuongoza mkutano wa Wote, suala la ubabe wa kisiasa likijitokeza wazi.

Magavana wa kaunti tatu za Ukambani wamekuwa wakifanya mikutano mara kwa mara huku wakimsuta Kalonzo kwa kuipotosha Jamii ya Akamba kisiasa, ahadi zao zikiwa kuwanusuru wakazi mikononi mwa Kalonzo.