array(0) { } Radio Maisha | WHO imetangaza Virusi vya Corona kuwa Janga la Kimataifa la Dharura la Afya

WHO imetangaza Virusi vya Corona kuwa Janga la Kimataifa la Dharura la Afya

WHO imetangaza Virusi vya Corona kuwa Janga la Kimataifa la Dharura la Afya

Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza Virusi vya Corona kuwa Janga la Kimataifa la Dharura la Afya. Mkurugenzi Mkuu wa WHO Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hatua hiyo inatokana na kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo hadi katika mataifa mengine.

Akizungumza baada ya mkutano wa kamati ya shirika hilo la WHO, Daktari Ghebreyesus amesema wasiwasi Mkuu ni Virusi vya Corona kusambaa hadi katika mataifa yasiyo na uwezo wa kuvikabili. Amesema Uchina ina uwezo mkubwa wa kushughulikia waathiriwa ,hivyo basi ana imani kwamba vitakabiliwa.

Tangazo la WHO,  linafuatia hatua ambapo baadhi ya watu ambao hawajasafiri hadi Uchina kuanza kuonesha dalili za virusi hivyo vya Corona.

Hayo yanajiri huku mkurugenzi mkuu huyo,  akisema idadi ya watu waliofariki dunia kufuatia kusambaa kwa Corona ikifikia mia mbili kumi na wanane huku visa tisini na vinane vikiripotiwa nje ya Uchina.

Tangazo la WHO,  linamaanisha kwamba mataifa yanafaa kujitahadhari ili kuzuia maambukizi zaidi. Kwa mfano; yanaweza kuchukua hatua ya kuifunga mipaka yao,  kusitisha safari za ndege hadi uchina, kuwafanyia ukaguzi wasafiri wote wanaoingia katika mataifa yao, miongoni mwa mikakati mingine.

Humu nchini, kila msafiri anayeingia nchini kutoka taifa lolote lile atakaguliwa ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo vya Corona. Amesema Waziri wa Afya Cisly Kariuki. Waziri Kariuki ameendelea kusisitiza kwamba mikakati ya kutosha imewekwa kukabili kusambaa kwa virusi hivyo, huku akirejelea kauli ya awali kuwa hakuna tishio lolote kufikia sasa kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa virusi hivyo nchini.

Kauli ya serikali imejiri wakati ambapo Chama cha Wafanyakazi wa Mashirika ya Ndege , kikitishia kushiriki mgomo au kususia kazi katika Ndege zinazoelekea Uchina ili kuushinikiza usimamizi wa shirika hilo kupiga marufuku safari za Uchina. Katibu Mkuu wa chama hicho, Moss Ndiema amesema shughuli ya kuwakagua wasafiri haitoshi.

Ikumbukwe Shirika la Ndege Kenya Airways, likikataa kusitisha safari zake kuelekea Uchina.Tayari mataifa kadhaa yakiwamo Uganda na Ethiopia yametangaza Corona kuwa janga la kitaifa, hivyo basi kuwashauri raia wake kutosafiri kwenda Uchina au kuingia kutoka mataifa hayo.

Hayo yanajiri huku matokeo ya sampuli za mwanafunzi aliyewasili nchini kutoka Uchina yakisubiriwa.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali Kanali Mustaafu Cyrus Oguna, amesema hali ya mwanafunzi huyo inaendelea kuimarika .

Mwanafunzi huyo anazuiliwa kwenye chumba maalum katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,  akisubiria matokeo kabla ya kuruhusiwa kuondoka.