array(0) { } Radio Maisha | Kundi la Kieleweke ladai kuwapo kwa mipango ya kumbandua Rais Kenyatta mamlakani

Kundi la Kieleweke ladai kuwapo kwa mipango ya kumbandua Rais Kenyatta mamlakani

Kundi la Kieleweke ladai kuwapo kwa mipango ya kumbandua Rais Kenyatta mamlakani

Mkutano wa Kundi la Viongozi wa Tangatanga uliofanyika mjini Naivasha ulilenga kuanzisha mchakato wa kumbandua mamlakani Rais Uhuru Kenyatta, lisema kundi la viongozi wa Kieleweke.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo y abunge, viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, Mbunge wa Kieni Kanini Kega, Mwakilishi wa Kike wa Homabay na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala miongoni mwa wengine, wamedai kwamba Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti ndiye mwanzilishi wa mchakato huo licha ya kujukumiwa kuwaongoza viongozi wenza katika kufanikisha ajenda ya serikali.

Wakati uo huo, viongozi hao wamewashtumu wabunge wa Kundi la Tangatanga kwa madai ya kuwa na unafiki mkubwa katika mchakato wa BBI. Seneta wa Kakamega Cleophus Malala akisema kuwa licha ya wao kutangaza kuunga mkono mikutano ya BBI, walitangaza tarehe nane mwezi ujao kuwa watafanya mkutano wao wa BBI hata baada ya ratiba ya mikutano hiyo kuonesha kuwa unapaswa kufanyika tarehe ishirini na nane.

Malala amewaonya wanasiasa hao wa Tangatanga kuwa hawatapewa nafasi ya kuhutubu wakati wa mikutano ya BBI, akidai kuwa wanalenga kuipinga na kwamba uamuzi wao wa kuhudhuria mikutano inayoendelea una ajenda fiche.

Aidha Gladys Wanga kwa upande wake amedai kwamba wabunge hao waliwahadaa Wakenya kwamba waliohudhuria mkutano wa Naivasha walikuwa takribani mia moja sabini, akisema kwamba walikuwa sabini na wanane pekee.

Amesisitiza kwamba mikutano halisi ya BBI ni ile ambayo inaogozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga na kwamba hakuna mwingine ambaye anaweza kuitisha mikutano hiyo.

Ikumbukwe awali mkutano wa Naivasha ulidaiwa kuwa wa wabunge wa Chama cha Jubilee kabla ya kubainika kwamba viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vingine pia walihudhuria. Aidha Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alisema chama hicho hakiutambui mkutano huo kuwa wa wajumbe wake.