array(0) { } Radio Maisha | Noordin Hajji aelezea matumaini ya kuhukumiwa kwa washukiwa wa ufisadi mwaka huu

Noordin Hajji aelezea matumaini ya kuhukumiwa kwa washukiwa wa ufisadi mwaka huu

Noordin Hajji aelezea matumaini ya kuhukumiwa kwa washukiwa wa ufisadi mwaka huu

Mkuu wa Mashtaka ya Umma, DPP Noordin Hajji ameahidi kukamilishwa kwa kesi mbalimbali za ufisadi mwaka huu na washukiwa wakuu kuhukumiwa. Hajji amesema ofisi hiyo imejitolea kuhakikisha kwamba haki inatendeka katika kesi mbalimbali za ufisadi ambazo imekuwa ikishughulikia.

Hajji hata hivyo amewataka wananchi  kutoilaumu ofisi hiyo endapo watu watakaopatikana na hatia wataamua kukata rufaa kuhusu maamuzi dhidi yao akisema ni haki ya kikatiba kwa  yeyote anayeshtakwia kuwasilisha rufaa iwapo atahisi hajatendewa haki.

Kwa mara nyingine mkuu huyo wa mashtaka ametaka kuheshimiwa kwa maagizo ya mahakama ambayo hutolewa mara kwa mara hasa kufuatia kukithiri kwa visa vya ukiukaji wa maagizo yenyewe. Wakati uo huo ameahidi kutwaliwa kwa mali zaidi inayomilikiwa kinyume na sheria akisema kufikia sasa hazina maalum iliyofunguliwa na ofisi yake imezihifadhi shilingi bilioni 2.9 ambazo zilitwaliwa kutoka kwa waliozipata kwa njia isiyo halali.

Kwa upande wake mkuu wa ujumbe wa mabalozi wa Umoja wa Bara Uropa, EU ambao wako ziarani nchini, Simon Mordue amesema umoja huo utaendelea kuisaidia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi. Mordue ameelezea imani kwamba washukiwa wakuu wa ufisadi watahukumiwa mwaka huu.

Hapo jana wajumbe wa EU walifanya kikao na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC ambapo walimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi za kukabili ufisadi. Aidha walitangaza kuwekeza shilingi billioni 3 katika mpango wa kuisadia Kenya kukabili ufisadi. Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Twalib Mbarak kwa upande wake alikashifu  madai kuwa  tume hiyo EACC haijawajibika katika vita dhidi ya ufisadi akisema kati ya mwaka 2018 -2019 kesi 78 za ufisadi ziliwasilishwa mahakamani na 51 kufanyiwa uamuzi.