array(0) { } Radio Maisha | Rais Kenyatta asema BBI haisababishi migawanyiko inavyodaiwa

Rais Kenyatta asema BBI haisababishi migawanyiko inavyodaiwa

Rais Kenyatta asema BBI haisababishi migawanyiko inavyodaiwa

Rais Uhuru Kenyatta ameweka wazi kwamba hamuungi wala kumtenga yeyote kupitia Mpango wa Upatanishi, BBI.

Wakati wa hotuba yake mapema leo katika Ikulu ya Mombasa akiwa pekee bila kuandamana na naibu wake William Ruto jinsi ilivyokuwa mwanzoni mwa utawale wao, Rais Kenyatta amesema kwamba lengo la mapatano baina yake na Raila Odinga ni kuwaunganisha Wakenya pamoja na kukabili masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiibuka hususan baada ya kila uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, Rais amekwepa kujibu moja kwa moja tetesi kwamba mpango mzima wa BBI ni kulenga kumwezesha kusalia madarakani baada ya muhula wake wa pili kukamilika.

Kuhusu masuala ya ufisadi, Rais amesisitiza kwamba Serikali Kuu imejitolea kuhakikisha maafisa fisadi katika serikali yake wanakabiliwa, huku akiitaka Idara ya Mahakama kuzifuatilia kwa makini kesi za ufisadi zinazowasilishwa katika mahakama za humu nchini.

Akitoa mfano wa hivi majuzi, ambapo ndugu wawili wa familia ya Akasha walihukumiwa nchini Marekani, mwaka mmoja tu baada ya kukamatwa kwa kuhusishwa na ulanguzi wa dawa za kulevya, Rais amesema usikilizaji wa kesi za ufisadi nchini unastahili kuharakishwa. Aidha, kwa mara nyingine amekana madai kwamba vita dhidi ya ufisadi vinawalenga watu fulani.

Wakati uo huo mamilioni ya Wakenya, wamepata afueni baada ya Rais kumesitisha kwa muda mapendekezo mapya kuhusu Bima ya Kitaifa ya Afya, NHIF akisema kwamba sharti majadiliano yafanyike kwanza miongoni mwa washikadau.

Wakati uo huo, Rais amesema serikali kuu na zile za kaunti zimeendelea kutii agizo la kuhakikisha kwamba zinalipa madeni zinayodaiwa, huku akisema kufikia mkesha wa mwaka mpya, asilimia sabini ya madeni hayo yamelipwa kufuatia agizo lake huku akisema kwamba asilimia 30 yaliyosalia yatalipwa kufikia mwezi ujao.