array(0) { } Radio Maisha | Kiunjuri atimuliwa kutoka kwa Baraza la Mawaziri

Kiunjuri atimuliwa kutoka kwa Baraza la Mawaziri

Kiunjuri atimuliwa kutoka kwa Baraza la Mawaziri

Rais Uhuru Kenyatta amefanya mabadiliko makuu katika baraza lake la mawaziri ambapo amemfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, kisha kuwateua watu wawili kujiunga na Baraza la Mawaziri na kuwapa uhamisho mawaziri wengine sita.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Peter Munya ndiye waziri mpya wa Kilimo huku Ukur Yatani akiteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, baada ya kushikilia wadhifa huo kikaimu kwa muda tangu aliyekuwa Waziri Henry Rotich kuondolewa kufuatia tuhuma za ufisadi. Tayari Yattani ametuma taarifa ya kumshukuru Rais kwa kuwa na imani na utendakazi wake.

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Cecily Kariuki aidha amehamishiwa Wizara ya Maji, wadhifa wake ukichukuliwa na aliyekuwa Seneta wa Nyeri, Mutahi Kagwe ambaye uteuzi wake kwanza utajadiliwa na Bunge la Kitaifa. Aidha Betty Maina, ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda japo hatma yake pia i mikononi mwa Bunge la Kitaifa ambalo litajadili kumwidhinisha ama kupinga uteuzi wake.

Aidha Rais amefanya mabadiliko ya makatibu wa wizara huku watu sita wakiteuliwa kushikilia nyadhifa hizo na wengine wanane kupewa uhamisho. Walioteuliwa ni  Balozi John Weru kuwa Katibu wa Biashara, Dr. Julius Jwan aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa KICD, Katibu wa Mafunzo ya Ufundi Anwai, Mary Kimonye Huduma kwa Umma, Balozi, Simon Nabukwesi ameteuliwa kuwa Katibu wa Elimu ya Vyuo Vikuu na Utafiti, Solomon Kitungu Katibu wa Uchukuzi huku Enosh Momanyi Onyango akiteuliwa kuwa Katibu wa Mipango. Makatibu waliokuwapo aidha amehamishwa huku Joe Okudo akiteuliwa kuwa Katibu wa Wizara ya Michezo na Colleta Suda akateuliwa kuwa Katibu wa Jinsia.

Rais Kenyatta vilevile, amewateua Makatibu Wakuu wa Utawala huku Hussein Dado akiteuliwa kuhudumu katika Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi. Partrick Ole Ntutu, aidha ameteuliwa kuhudumu katika Wizara ya Leba. Mwanasiasa Wavinya Ndeti ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Uchukuzi.

Rais Kenyatta ametangaza kwamba miongoni mwa walioteuliwa kuwa makatibu wakuu wa utawala ni vijana wasiozidi umri wa miaka thelathini huku akitoa changamoto kwao kujifunza mengi kutoka kwa wakuu wao na wenye uzoefu mkubwa serikalini. Aidha, idara ya masuala ya vijana iliyokuwa chini ya Wizara ya Huduma za Umma sasa itakuwa chini ya Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano, ICT huku vyama vya ushirika vikiwekwa chini ya Wizara ya Kilimo.