array(0) { } Radio Maisha | Mudavadi na Wetangula wataka kuchapishwa kwa nakala zaidi za ripoti ya BBI

Mudavadi na Wetangula wataka kuchapishwa kwa nakala zaidi za ripoti ya BBI

Mudavadi na Wetangula wataka kuchapishwa kwa nakala zaidi za ripoti ya BBI

Kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi ametoa wito kwa Mwenyekiti wa Jopo la Mpango wa Upatanishi, BBI Yusuf Hajji kuwapa Wakenya ratiba kamili ya kuishughulikia ripoti iliyoandaliwa na jopo hilo kuhusu marekebisho ya Katiba wanayohitaji wananchi. Akizungumza katika Kaunti ya Kakamega, Musalia aidha amesema masuala ambayo hayajaangazia katika ripoti hiyo yanastahili kuwekwa wazi ili yajumuishwe katika ripoti ya pili iwapo itaandaliwa.

Musalia hata hivyo amelalamikia kutokuwapo kwa nakala za kuwasambazia wananchi ili waisome na kuilewa vyema ripoti hiyo akisema hali hiyo huenda ikahujumu lengo la maandalizi ya ripoti yenyewe.

Kinara wa Chama cha Ford Kenya, Moses Wetangula vilevile ametilia mkazo suala la kuchapishwa kwa nakala zitakazosambaziwa wananchi.

Wakati uo huo, Wetangula amewashtumu wanasiasa wanaoipigia debe ripoti ya Jopo la Mpango wa Upatanishi, BBI kwa manufaa binafsi. Wetangula amesema wanasiasa wengine wanaichukulia ripoti hiyo kuwa ya kunufaisha malengo yao binafsi japo amesema mpango huo hautafaulu.

Wetangula aidha amesema licha ya kwamba masuala tisa yaliangaziwa katika maandalizi ya ripoti hiyo, wanasiasa wamelizingatia zaidi suala la ugavi wa nyadhifa za uongozi ambalo wanalipigia upatu ishara kwamba hawamjali mwananchi.