array(0) { } Radio Maisha | Raila ajiondolea lawama kuhusu masaibu ya Miguna

Raila ajiondolea lawama kuhusu masaibu ya Miguna

Raila ajiondolea lawama kuhusu masaibu ya Miguna

Kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga amejiondolea lawama kuhusu masaibu yanayomkumba Wakili Miguna Miguna kuhusu kurejea kwake nchini.

Raila amesema alifanikiwa kumshauri Rais Uhuru Kenyatta wakati wa mapatano kati yao, kumruhusu Miguna kurejea nchini ikizingatiwa kwamba alikuwa mmoja wa wanachama wa NASA na kwamba ndiye aliyemwapisha Raila kuwa Rais wa Wananchi.

Odinga amejiondolea lawama kwamba amesalia kimya huku mashirika mbalimbali ya kimataifa ya ndege yakikataa kumsafirisha kuja Nairobi. Kwa mujibu wa Raila, alifanya kila aliloweza kuhakikisha kwamba wakili huyo anarejea nchini kutoka Canada ambako alifurushwa mwezi Februari miaka miwili iliyopita. Aidha, amemlaumu Miguna kwa kuwa msumbufu.

Kauli ya Raila inajiri wakati Miguna akiendelea kuwashutumu Uhuru na Odinga akidai wamechochea kuzuiwa kwake kusafiri kuja nchini Kenya.