array(0) { } Radio Maisha | Mahakama yaagiza kuzuiliwa kwa mshukiwa wa Al Shabaab aliyejisalimisha

Mahakama yaagiza kuzuiliwa kwa mshukiwa wa Al Shabaab aliyejisalimisha

Mahakama yaagiza kuzuiliwa kwa mshukiwa wa Al Shabaab aliyejisalimisha

Mahakama imeagiza kuzuiliwa kwa siku kumi kwa mwanamume aliyekiri kuwa mwanachama wa Kundi Gaidi la Al Shabaab aliyerejea kutoka Somalia kisha kujiwasilisha katika kanisa moja jijini Mombasa Ijumaa wiki iliyopita.

Hakimu Mkuu, Ednah Nyaloti ameagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa kwa muda huo ili kutoa fursa kwa  upande wa mashtaka kufanya uchunguzi dhidi yake. Uamuzi huo umefuatia ombi lililowasilishwa na Mwendesha Mashtaka, Eric Masila ambaye aliomba mahakama muda ili kukamilisha uchunguzi.

Ameiambia mahakama hiyo kwamba mshukiwa huyo alijiwasilisha kanisani Ijumaa wiki iliyopita na kukiri kuwa mwanachama wa Al Shabaab huku akimsihi kasisi kumwombea. Hata hivyo alikabidhiwa kwa polisi ambao wamekuwa wakimzuilia.

Mwendesha Mashtaka ameiomba mahakama hiyo kutoliweka wazi jina la mshukiwa kwa sababu za kiusalama ikizingatiwa kwamba ataisadia Idara ya Usalama na taarifa muhimu kuhusu kundi hilo la kigaidi. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tarehe ishirini na tatu mwezi huu.

Kesi hii inajiri wakati ambako Kund la Al Shabaab limekuwa likitekeleza mashambulio kwenye baadhi ya maeneo humu nchini la hivi punde likiwa eneo la Saretho, Daadab ambapo wanafunzi wanne wameuliwa leo mwendo wa saa saba usiku. Eneo la Lamu pia limekuwa likikumbwa na mashambulio ya kigaidi katika siku za hivi karibu.