array(0) { } Radio Maisha | NIKO TAYARI, K’OGALLO WAJE

NIKO TAYARI, K’OGALLO WAJE

NIKO TAYARI, K’OGALLO WAJE

Kocha mkuu wa Posta Rangers fc Sammy Omollo ‘Pamzo’ ametia mahanjam katika mechi ya timu yake dhidi ya Gormahia itakayo chezwa siku ya jumapili mjini Narok.

Pamzo ambaye pia alikuwa mchezaji wa zamani wa Gormahia fc, alizungumza mapema wiki hii na idara ya michezo Redio Maisha huku akionesha ujasiri na ukakamavu.

“Nilikuwa na majeraha mengi sana na pia baadhi ya wachezaji wangu walikuwa wanahudumia marufuku za kadi nyekundu. Suleiman Ngotho naye alikuwa na Harambee Stars katika michuano ya CECAFA kule Uganda. Kikosi changu hakikuwa na mabeki ndio maana mechi mbili zilizopita sikuwa na ulinzi mzuri. Kwa sasa timu iko sawa na tumekuwa tukifanya mazoezi ipasavyo, Gormahia wapinzani wetu hawajakuwa wakifanya mazoezi kama sisi, jambo ambalo natumahi litatufaa jumapili.” Alijutia hali yake ya awali Pamzo, huku akifurahia ya sasa.

Posta Rangers ilifungwa na KCB mabao matano kwa moja mjini Machakos katika raundi ya 13 ligi kuu nchini KPL. Katika mechi hiyo, Pamzo alishuhudia mabeki kati wake wawili wakilishwa kadi nyekundu. Mechi iliyofuatia, Posta walitoka nyuma mabao matatu kwa moja na kupata sare ya mabao matatu kwa matatu dhidi ya Kariobangi Sharks, jambo ambalo lilimridhisha Pamzo.

“Timu yangu imekuwa na ulinzi bora zaidi ya timu yeyote ile katika ligi msimu huu. Mechi kumi za kwanza za msimu tulifungwa si zaidi ya mabao manne, lakini angalia mbili za awali tumefungwa ujumla wa mabao manane. Kwa sasa nafurahia kwa sababu vijana wangu wote wamerejea kambini na kikosi kiko imara. Gormahia watarajie hali ngumu, haitakuwa rahisi kupata alama dhidi yetu.” Pamzo alionesha ushujaa huku akiongezea kwamba lengo la Posta nikumaliza msimu huu katika nafasi ya nne bora.

Gormahia, mabingwa watetezi wa taji la KPL na pia mabingwa mara 18, watashuka dimbani, mjini Narok siku ya jumapili saa nane mchana dhidi ya Posta Rangers fc. Kisha baadaye, Posta itakuwa na kibarua tena dhidi ya mabingwa mara nne wa KPL, Ulinzi stars fc.

Posta, ambayo iko katika nafasi ya tisa baada ya mechi 13 na alama 18, ina matumaini ya kwamba ili kuiweka ndoto yake hai, lazima ipate alama zote tatu kutoka kwa Gormahia ambao wako kidedea kwa wingi wa mabao kwa alama 28, baada ya mechi 11. Tusker fc wako katika nafasi ya pili huku wakiwa na alama sawa na K’ogallo.

Ulinzi stars fc ambao watakuwa wapinzani wa Posta Rangers baada ya kivumbi cha wanabarua na wala samaki, wako katika nafasi ya tano, baada ya mechi 14 na alama 25. Sammy Omollo ‘Pamzo’ ana imani ya kwamba ili ndoto yake ya kumaliza katika nafasi ya nne bora itimie, lazima awabwage miamba hawa wawili wa soka nchini Kenya. Kutoka kwetu Redio Maisha, twamtakia kila la heri.