array(0) { } Radio Maisha | Hakuna Krismasi kwa wachezaji wangu; amesema Pamzo

Hakuna Krismasi kwa wachezaji wangu; amesema Pamzo

Hakuna Krismasi kwa wachezaji wangu; amesema Pamzo

Mkufunzi wa Posta Rangers fc Sammy ‘Pamzo’ Omollo amewatangazia wachezaji wake ya kwamba hawatakuwa na likizo fupi ya krismasi.

Akizunguma na idara ya michezo Redio Maisha mapema siku ya jumamosi, Pamzo hakusita kuonesha ukakamavu.

“Nina mechi ngumu zaidi mbele yangu baada ya krismasi. Mechi iliyopita baada ya kichapo cha KCB, tulienda saree ya K-Sharks, sasa ifuatayo ni Gormahia, kisha Ulinzi stars fc. Sioni kama nina nafasi ya kuenda likizo. Mechi ya Gormahia ni ngumu kwa sababu wale ni mabingwa watetezi, Ulinzi stars huwezi cheza nawo kama haujafanya mazoezi. Wale wanajeshi wana maguvu ya ajabu,” alisema Pamzo huku akizidisha mazoezi kwa wachezaji wake walioko kambini kwa sasa.

KCB iliwacharaza Posta Rangers fc mabao matano kwa moja baada ya mabeki wa Posta wawili kuoneshwa kadi nyekundu. Baada ya hapo Posta rangers ilienda sare ya mabao matatu kwa matatu na Kariobangi sharks.

“Nimekuwa na shida na ulinzi wangu, ukiangalia mechi kumi za kwanza za msimu timu yangu ndio iliyokuwa na ulinzi bora zaidi katika KPL. Lakini baada ya majeraha ya hapa na pale, kadi nyekundu na Suleiman Ngotho kuita kwenye timu ya taifa, nimekuwa na uchache wa mabeki. Sasa nina matumaini kabla ya mechi ya K’ogallo na Ulinzi stars, vijana watakuwa imara. Sisi ukiangalia hali yetu, hatuna muda wa sherehe za krismasi, ni kazi tu. Krismasi ni siku kama siku nyingine yeyote, lakini kazi ilioko mbele yako ndio itakulipia kodi ya nyumba,” aliwashauri wachezaji wake Pamzo.

Posta Rangers yake Pamzo kwa sasa iko katika nafasi ya nane baada ya mechi 13 huku wakiwa na alama 18. Wapinzani wao K’ogallo wanashikilia nafasi ya nne baada ya mechi 10 na alama 25. Kisha mechi itakayofuatia niya Ulinzi stars ambao wako katika nafasi ya sita, baada ya mechi 13 na alama 22.

Sammy ‘Pamzo’Omollo ambaye alishinda taji la KPL akiwa mkufunzi wa Tusker fc msimu wa 2010/2011 ana azimio la kushinda tena taji hilo. Ni madhumuni yake ya kwamba bidii kutoka kwake, kamati yake ya kiufundi na wachezaji wake itawazalia matunda mema. Kutoka kwetu meza ya michezo Redio Maisha, twamtakia kila la heri na krismasi yenye fanaka.