array(0) { } Radio Maisha | Yaliyomo katika sheria kuhusu namna ya kuifanyia Katiba marekebisho
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Yaliyomo katika sheria kuhusu namna ya kuifanyia Katiba marekebisho

Yaliyomo katika sheria kuhusu namna ya kuifanyia Katiba marekebisho

Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi ameibua mjadala baada ya kusema kwamba jinsi Ripoti ya Jopo la Upatanishi, BBI ilivyo, haiwezi kushughulikiwa na Bunge la Kitaifa. Muturi amesema kwamba bunge halikuhusishwa wakati wa kuandaliwa kwa ripoti hiyo, hivyo basi itakuwa vyema kuirejesha kwa Wakenya waliohojiwa wakati wa kukusanywa kwa maoni ya BBI. Je, matamshi ya Muturi yana misingi ya kisheria ama yamechochewa kisiasa

Katiba ya Kenya vifungu vya 256 na 257 ni bayana kuhusu namna marekebisho ya katiba yanavyoweza kufanywa. Kifungu cha 256 kinazungumzia marekebisho ya katiba kupitia bunge huku kile cha 257 kikizungumzia marekebisho kupitia msukumo wa wengi yaani, Popular Initiative.

Tukitoa mfano wa marekebisho yaliyopendekezwa na Kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance, Ekuru Aukot, alilenga kutumia msukumo wa wengi ili kufanikisha marekebisho ya katiba.

Mfumo huo una masharti haya;

- Anayelenga kufanikisha marekebisho ya katiba ni sharti akusanye saini za wapiga-kura takriban milioni moja.

-Anayelenga marekebisho hayo kisha anaweza kuyajumuisha maoni ya wananchi kisha aandae mswada wenye mapendekezo hayo.  

- Hatua inayofuata ni kuuwasilisha mswada huo pamoja na saini milioni moja za wapigakura kwa Tume ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu la kuthibitisha iwapo saini zilizokusanywa ni halali.

-Baada ya kuzithibitisha na kuziidhinisha, itawasilisha mswada huo kwa mabunge yote ya kaunti ili ujadiliwe kwa kipindi cha miezi mitatu.

-Baada ya kila kaunti kuujadili mswada huo na kuidinisha ama kuuangusha, itauwasilisha kwa Spika wa Bunge la Kitaifa na mwenzake wa Seneti pamoja na cheti cha kuonesha iwapo mswada wenyewe ulipitishwa ama la.

- Iwapo mswada huo utakuwa umeidhinishwa na zaidi ya kaunti 24, basi utajadiliwa na Bunge la Kitaifa na Seneti. Aidha iwapo utakosa kufikisha idadi hiyo ina maana umefeli.

- Aidha, ukiidhinishwa na asilimia kubwa ya kaunti, utajadiliwa na Bunge la Kitaifa vilevile Seneti. Ikiwa mojawapo ya mabunge haya mawili yatauangusha mswada wenyewe hata kama uliidhinishwa na asilimia kubwa za kaunti, utapelekewa wananchi ili waamue kupitia kura ya maamuzi.

Mfumo wa pili wa kufanya marekebisho ya katiba ni ule ulio katika kipengee cah 256 ambao unalihusisha bunge.

Kuambatana na utaratibu uliofafanuliwa katika kipengee hiki;

- Mswada wenye mapendekezo ya marekebisho ya katiba unaweza kuwasilishwa katika bunge lolote lile, liwe la Kitaifa ama Seneti.

-Mswada huo unaweza kuzungumzia marekebisho katika sheria fulani ambazo zilibuniwa kupitia katiba.

-Mswada huo kisha utajadiliwa mara moja na kusubiri siku tisini kabla ya kujadiliwa tena kwa mara ya pili. Ili kuujadili tena, nilazima uwe uliidhinishwa mara ya kwanza ulipojadiliwa.

Aidha, mswada wenyewe utakapoidhinishwa na mabunge yote mawili na zaidi ya thuluthi mbili ya wabunge, mabunge hayo yatachapisha mswada huo ili kuwapa wananchi fursa ya kuudhurusu na kutoa maoni yao kuhusu marekebisho ya katiba yanayopendekezwa.

-Kitakachofuata ni maspika wa mabunge yote mawii kuwasilisha mswada huo kwa Rais ili kuudhinisha na kuuchapisha. Vilevile watawasilisha cheti cha kuonesha uliidhinishwa na mabunge yao. Rais atakapoudhinisha, atahakikisha umechapishwa kwa kipindi cha siku thelathini kuwa sheria.

Hata hivyo iwapo mswada wenyewe unagusia kipengele cha 255 cha katiba, basi ni sharti mswada huo kabla ya Rais kuudhinisha, aiagize Tume ya Uchaguzi kufanya kura ya maamuzi kwa kipindi cha siku tisini.

Kipengee hicho cha 255 kinaagiza kwamba kura ya maamuzi itafanyika endapo marekebisho yanayolengwa ni kubadili mfumo wa uongozi, huduma za bunge, mipaka na kadhalika.

Kura ya maamuzi itakapofanyika na uidhinishwe, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi atamjulisha Rais kwa kipindi cha siku thelathini kwamba uliidhinishwa hivyo kumpa Rais uhuru wa kuutia saini kuwa sheria.

Ikizingatiwa vigenzo vya kisheria vilivyopo, ina maana kwamba ripoti ya BBI haikuandaliwa kwa vigezo vya sheria na huenda ikalazimika ripoti hiyo ibadilishwe kuwa mswada kisha kuwasilishwa kwa kuzingatia katiba niliyoyafafanua hapo awali.