array(0) { } Radio Maisha | Je, ripoti ya BBI ijadiliwe Bungeni au wananchi wahusishwe?

Je, ripoti ya BBI ijadiliwe Bungeni au wananchi wahusishwe

Je, ripoti ya BBI ijadiliwe Bungeni au wananchi wahusishwe

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Malumbano yameendelea kushuhudiwa kuhusu jinsi ripoti hiyo ya BBI itakavyotekelezwa.

Baadhi ya viongozi wanaunga mkono pendekezo la Naibu wa Rais William Ruto kwamba ripoti hiyo ijadiliwe Bungeni huku baadhi wakipinga na kushinikiza lile la Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kwamba inastahili kupelekwa kwa mwananchi.

Chama cha ODM kinasema kwamba hakitakubali mapendekezo yoyote ambayo hayatawahusisha wananchi kupitia kura ya maamuzi. Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga amesema kwamba watazidi kushinikiza mchakato wa utekelezaji wa ripoti hiyo utekelezwe kwa kuhusisha umma na washikadau wote, maarufu Popular Initiative, ili kumpa kila mmoja kutoa maoni yake.

Kauli sawa na hiyo imetolewa na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM huku akisema Bunge haliwezi kutegemewa, kwani linaweza kushawishika kwa urahisi.

Aidha, kwa upande wao zaidi ya wabunge ishirini  wa kundi la Tangatanga wamesema wananchi wanastahili kupewa nafasi ya kujiamulia bila kushinikizwa na viongozi wa Kisiasa. Kimani Ngunjiri ni Mbunge wa Nyeri Mjini.

Akizungumzia suala lilo hilo, Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema wataisoma ripoti hiyo kabla ya kutoa mwelekeo, japo anaunga mkono Waziri Mkuu kutengewa mamlaka zaidi ya inavyopendekezwa.

Tayari BBI imeanza kupingwa na baadhi ya viongozi wanaosema haitawanufaisha Wakenya. Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Francis Atwoli licha yakuupigia debe mpango wa BBI awali amesema ripoti hiyo haiwezi kutekelezwa jinsi ilivyo. Kiongozi mwingine anayeipinga ni Seneta wa Narok Ledama ole Kina.