array(0) { } Radio Maisha | Yusuf Hajji aghadhabishwa na hulka za viongozi wakati wa uzinduzi wa BBI
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
×

Yusuf Hajji aghadhabishwa na hulka za viongozi wakati wa uzinduzi wa BBI

Yusuf Hajji aghadhabishwa na hulka za viongozi wakati wa uzinduzi wa BBI

Na Esther Kirong'

NAIROBI, KENYA, Mwenyekiti wa Jopo la Upatanishi, BBI Yusuf Hajji ameelezea kughadhabishwa na hulka za baadhi ya viongozi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya jopo hilo Jumatano wiki hii katika Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Akiwahutubia wanahabari wakati wa mkutano wa kutamatisha shughuli zao afisini tangu kuzinduliwa kwa jopo hilo, Hajji ambaye pia ni Seneta wa Garissa amesema BBI haikupanga ratiba ya watu kuzungumza kwani kazi yake ilikuwa ni kutoa ripoti kwa umma.

Ameelezea kusitikishwa na kauli ya Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed dhidi ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen. Amesema alishangazwa sana kwani kauli yake iliashiria kwamba hafla hiyo ilikuwa ya Chama cha ODM na wale waliokuwa wakiunga mkono Mapatano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Seneta huyo amesema baadhi ya viongozi walibaguliwa wazi huku wanachama wa BBI wakilaumiwa ilhali ratiba hiyo ilitolewa na Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi kwa ushirikiano na baadhi ya viongozi.

Aidha, Seneta Hajji amewasuta viongozi wanaopinga mapendekezo ya ripoti hiyo akisema wao hawakuegemea upande wowote bali waliyawasilisha maoni yaliotolewa na Wakenya. Amesema walipokuwa wakizunguka nchini, lengo lilikuwa kumridhisha Mkenya mlipa-kodi bali si wanasiasa wanaojali maisha yao wenyewe.

Sawa na Naibu wa Rais, William Ruto pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale, Hajji amesema ripoti ya BBI inaweza kujadiliwa bungeni na kupitishwa au kuangushwa.

Kulingana naye, serikali haina fedha za kubuni jopo jingine kuzunguka nchini ili kuijadili ripoti hiyo. Aidha amepuuza suala la katiba kufanyiwa marekebisho, akisema BBI haikupendekeza kufanywa kwa kura ya maamuzi hasa ikizingatiwa mapendekezo yote yaliotolewa yanaweza kujadiliwa katika mabunge yote mawili.