array(0) { } Radio Maisha | Ripoti ya BBI kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta na Raila
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Ripoti ya BBI kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta na Raila

Ripoti ya BBI kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta na Raila

Hatimaye Ripoti ya Jopo la Upatanishi BBI itawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga leo hii katika Ikulu hapa jijini Nairobi.

Ripoti hiyo ambayo imeibua mihemko ya kisiasa nchini aidha inafasiriwa kwamba huenda ikabilisha siasa za humu nchini hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga ripoti hiyo inalenga kuwaunganisha Wakenya vilevile kuhakikisha kuwa hakutakuwapo na umwagikaji wa damu kila baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, licha ya kuwa ripoti hiyo itakabidhiwa viongozi hao wawili kabla ya kuiweka wazi kwa umma Jumatano, kampeni za kuiunga mkono na kuipinga zimekuwa zikiendelea nchini na hata kusababisha kuchipuka kwa makundi manne ya wabunge yanayounga na yanayopinga.

Makundi ya Tangatanga ambalo ni la wabunge wa Kiume na lile la Inua Mama la Wabunge wa Kike yamekuwa yakiendeleza mijadala ya kuipinga ripoti hiyo kivyovyote vile kwa madai kuwa inalenga kubuni nafasi zaidi za uongozi serikali. Nayo makundi ya Kieleweke la wabunge wa Kiume na Embrace la wabunge wa kike, yamekuwa yakiipigia debe ripoti hiyo, wakidai kuwa ndiyo njia pekee ya kuunga mkono juhudi za Rais Kenyatta na Raila Odinga kuleta pamoja taifa hili.

Hata hivyo akizungumza katika Kaunti ya Bungoma Rais Uhuru Kenyatta aliwashauri viongozi kusitisha mijadala kuihusu na badala yake kusubiri kuwekwa wazi kisha kuisoma na kufanya maamuzi ya iwapo wataipinga au kuiunga mkono.

Kwa upande wake Kinara wa ODM Raila Odinga amekuwa akiitaja ripoti hiyo kuwa italeta mabadiliko makubwa katika uongozi wa taifa hili, mabadiliko ambayo kulingana naye yanalenga kutatua masaibu ya Wakenya kupitia marekebisho ya katiba.

Ni kufuatia kauli yake ambapo, viongozi wa Tangatanga na Inua Mama wamekuwa wakimkosoa wakidai kwamba, taifa hili haliwezi kukubali mageuzi ya uongozi kwa manufaa ya wachache. Naibu wa Rais William Ruto akisistiza kwamba ripoti hiyo inapaswa kuzingatia jinsi ya kumnufaisha Mkenya.

Ikumbukwe Jopo la Upatanishi BBI lilibuniwa kufuatia mwafaka wa mwezi wa machi mwaka 2018 kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga baada ya marudio ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 ambapo Mahakama ya Juu ilifutilia mbali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Baada ya Jopo hilo linaloongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Hajji kubuniwa, lilijukumiwa kukusanya maoni katika kaunti zote arubaini na saba kabla ya kuiandika ripoti hiyo. Hata hivyo licha ya Jopo hilo kuahidi kutoa ripoti hiyo mapema mwezi huu, Wakenya watalazimika kusubiri hadi kesho ambapo itawekwa wazi kwa umma katika Ukumbi wa Bomas hapa jijini Nairobi.