array(0) { } Radio Maisha | Amos Wako akana kuhusika ufisadi huku akiikosoa Marekani kwa kumwekea marufuku ya usafiri
×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Amos Wako akana kuhusika ufisadi huku akiikosoa Marekani kwa kumwekea marufuku ya usafiri

Amos Wako akana kuhusika ufisadi huku akiikosoa Marekani kwa kumwekea marufuku ya usafiri

Seneta wa Busia, Amos Wako ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amekana kuhusika katika ufisadi vilevile kuelezea kushangazwa kwake na hatua ya Marekani kuweka marufuku kwa mkewe na mwanawe dhidi ya kusafiri hadi nchini humo kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Akiwahutubia wanahabari kwa mara ya kwanza tangu kutolewa kwa marufuku hayo, Wako amesema Marekani haijaweka bayana madai dhidi yake hivyo kuitaka kutoa maelezo ya kina.

Wako aidha amesema ni jambo la kushangaza kuwekewa marufuku mengine miaka kumi baada ya yale ya awali, akisema huenda kuna njama fiche dhidi yake ambayo haifahamu. Ameeleza kwamba madai yaliyoibuliwa dhidi yake ya kuhusika ufisadi aliyashughulikia wakati alipokuwa Mwanasheria Mkuu.

Wakati uo huo, Wako ameghadhabishwa na hatua ya kuihusisha familia yake katika suala la marufuku ya usafiri hadi Marekani, akisema iwapo ni kweli kuna ufisadi aliyohusika, familia yake haistahili kuhusishwa kwa vyovoyte vile.

Kauli ya Wako imejiri siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC Eliud Wabukala kuzitetea idara za uchunguzi humu nchini kwa madai ya kuzembea katika kukabili ufisadi kiasi cha mataifa mengine kuhusika akisema marufuku dhidi ya Wako ni miongoni mwa matunda ya ushirikiano kati ya Marekani na Kenya katika vita dhidi ya ufisadi.

Wako alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya kwa muda wa miaka ishirini ambapo wakati wa kuhudumu kwake, kashfa mbalimbali za ufisadi zikiwamo za Angloleasing na GoldenBerg ziliripotiwa.