array(0) { } Radio Maisha | Mkenya Lonyangata, ameweka rekodi nyingine tena kule Shanghai

Mkenya Lonyangata, ameweka rekodi nyingine tena kule Shanghai

Mkenya Lonyangata, ameweka rekodi nyingine tena kule Shanghai

Paul Kipchumba Lonyangata, mapema Jumapili alishinda mbio za masafa marefu za kimataifa za Shanghai yaliyofanyika Uchina.

Mbio hizo za barabarani zimeidhinishwa na shirikisho la riadha duniani IAAF na kuorodheshwa kati ya zile zenye hadhi ya juu zaidi ulimwenguni.

“Nilikimbia mara ya mwisho hapa miaka minne iliyopita. Imekuwa muda, lakini hakuna mkimbiaji yeyote ambaye ameweza kuivunja rekodi yangu ya hapo awali. Nilitamani sana niivunje rekodi yangu mwenyewe lakini kijoto cha Uchina kili nilemea. Mazingira yamekuwa tofauti mwaka huu ukilinganisha na mara ya mwisho nilipo shindana hapa 2015.” Lonyangata alizungumza kwa uchache.

Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 26, alionesha ubabe wake alipo tengana na wenzake baada ya kilometa 35. Mazingira yalibadilika na vipimo vya joto kuongezeka kutoka nyuzi 15 hadi 20 lakini Lonyangata aliongoza hadi mwisho. Alimaliza mbio hizo za barabarani kwa muda wa masaa mawili, dakika 28 na sekunde 11, sekunde 57 nyuma ya rekodi ambayo aliiweka mwaka wa 2015.

“Kila kitu ni bidi tu. Nimekuwa nikifanya mazoezi kila uchao na matumaini yangu yalikuwa ni kuivunja hii rekodi tena. Lakini ndio hali ya maisha, nitajaribu tena siku nyingine, sitakata tamaa,” alionesha ujasiri Lonyangata.

Mwaka wa 2015, aliweka rekodi ya muda wa 2: 07: 14 katika mbio hizo za jiji la Shanghai.

Mwaka jana, Lonyangata alikuwa mwanariadha wa kwanza kutetea ubingwa wa mbio za barabarani za jiji la Paris, Ufaransa ambazo alizishinda mwaka juzi. Lakini mwaka huu mambo yalimwendea upogo alipokuwa anasaka taji lake la tatu jijini Paris mfululizo.

“Paris kulikuwa na changamoto si haba, lakini kwa neema zake mwenyezi Mungu niliweza kushiriki japo sikushinda. Wiki mbili kabla ya mashindano hayo, niliumia mkono wangu na kuelekea Italia kwa matibabu. Huko nilifanyiwa upasuaji. Nilimaliza mbio za Paris kwa  muda wa  2:07:29. Haikuwa mbaya nilivyo dhania maanake nilikuwa na siku tatu tu za maandalizi pekee,” alikiri Lonyangata, mzawa wa Pokot magharibi.

Jumapili, Shanghai, Uchina, mbio hizo za masafa marefu zilikuwa na mibabe 12 ambao walibanana bega kwa bega kilometa tano za kwanza kwa muda wa dakika 14 na sekunde 57. 

Wanaume hao waligonga muda wa dakika 29 na sekunde 58 walipofika kilometa kumi. Baada ya kilometa 15, viongozi hao 12 walibisha muda wa dakika 45 na sekunde moja, sekunde 47 mbele ya rekodi iliyowekwa wakati wa awali kabla ya mshindi wa leo.

Baada ya kilometa 20, bado walikuwa sekunde sita mbele kwa muda wa rekodi hiyo ya awali. Lakini Lonyangata aliwazidia ubavu walipofika kilometa 35 na kushinda mbio hizo.

Mkenya huyo sasa atarejea nchini na kuutuliza mwili wake kwa mapumziko anapojiandaa kwa sherehe za krismasi na familia yake. Bado ana matumaini ya kushiriki katika mbio za kimataifa duniani na kuipeperusha bendera ya Kenya siku moja. Kwetu sisi hapa Redio Maisha, twa mtakia kila la heri.